Chanjo ya pili iliyotegenezwa Iran kufanyiwa majaribio ya mwanadamu wiki ijayo
Chanjo ya pili ya Corona au COVID-19 iliyotengenezwa Iran ambayo inajulikana kama COV-Pars itaanza kufanyiwa majaribio ya mwanadamu wiki ijayo.
Kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Utafiti na Teknolojia katika Taasisi ya Chanjo ya Razi Dkt. Mohammad Hassan Fallah amesema wanaotaka kushiriki katika awamu ya kwanza ya majaribio wanaweza kujisajili. Amesema hadi sasa watu zaidi ya 100 wamejitolea kushiriki katika duru hii ya kwanza ya majaribio ya wanaadamu ya chanjo hiyo
Amesema watu 133 watafanyiwa majaribio katika awamu hii ya kwanza.
COV-Pars ni chanjo ya kwanza ya aina yake ambayo huingizwa mwilini kupitia kudungwa na pia kupitia kupumua kwa pua.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni kundi la utafiti wa chanjo ya virusi vya corona ya Iran inalojulikana kwa jina la 'COVO-Iran Barakat' limetangaza kuwa chanjo hiyo iko tayari kwa ajili ya awamu ya pili ya majaribio kwa wanadamu.

Mtaalamu anayesimamia awamu mbalimbali za majaribio ya chanjo ya virusi vya corona ya COVO-Iran Barakat, Minoo Mohraz amesema kwamba, matokeo ya majaribio ya chanjo hiyo ni mazuri sana na kuongeza kuwa, baada ya kufanyika kikamilifu zoezi la awamu ya kwanza, yumkini wiki ijayo kukaanza awamu ya pili na kuchunguza taathira zake kwa mwanadamu.
Afisa huyo wa masuala ya utafiti na teknolojia wa Wizara ya Afya ya Iran ameongeza kuwa, chanjo ya corona ya Cuba ambayo imepangwa kuzalishwa kwa kushirikiana na Iran imekamilisha awamu ya kwanza na ya pili nchini Cuba na awamu ya tatu ya majaribio yake ambayo itashirikisha watu baina ya 30 hadi 40 elfu, itafanyika nchini Iran na Cuba kwa wakati mmoja.
Wakati huo huo Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ijuma alitangaza kuwa, chanjo ya Corona au COVID-19 ya Sputnik V ya Russia sasa itaanza kutengenezwa hapa nchini.
Akizungumza na Shirika la Habari la IRNA, Mahmoud Vaezi, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Iran alisema sasa mbali na kuwa Iran inanunua moja kwa moja chanjo ya Sputnik V kutoka Russia chanjo hiyo pia itaanza kutegenezwa hapa nchini kufuatia mapatano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili.