Zarif: Iran italiunga mkono taifa linalodhulumiwa la Yemen
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran inaunga mkono harakati yoyote ambayo itapelekea kuhitimishwa hujuma dhidi ya taifa la Iran.
Katika mahojiano na Televisheni ya Al Masira, Zarif amesema jitihada za kuhitimisha mgogoro wa Yemen zinaendelea. Amesisitiza kuwa Iran inaunga mkono harakati yoyote yenye lengo la kuhitimisha mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen.
Zarif ameongeza kuwa, utangulizi wa kutatuliwa mgogoro wa Yemen, ni usitishwaji vita na kuondolewa mzingiro Yemen ili kuhitimisha maafa ya kibinadamu.
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono taifa la Yemen na mapambano yake na akasisitiza kuwa uungaji mkono huo ni katika fremu ya udharura wa kuunga mkono wanaodhulumiwa.
Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah.
Harakati hiyo imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ambapo imeleng mara kadhaa vituo vya kusafisha mafuta na pia viwanja vya ndege vinavyotumiwa na jeshi vamizi la utawala huo wa kifalme.
Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo..