Ulaya na JCPOA; sharti la Iran la kurudi kwenye Protokali ya Ziada
(last modified Thu, 25 Feb 2021 17:04:25 GMT )
Feb 25, 2021 17:04 UTC
  • Ulaya na JCPOA; sharti la Iran la kurudi kwenye Protokali ya Ziada

Jibu na radiamali ya pande za Ulaya na Marekani kwa hatua ya Iran ya kusimamisha utekelezaji wa hiari wa Protokali ya Ziada ya Mkataba unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia y NPT ni ya kutafakariwa na inaonesha muelekeo na mtazamo usio wa kimantiki wa pande hizo.

Kusimamisha utekelezaji wa hiari wa Protokali ya Ziada si jambo lililofurahiwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na wanachama wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; na ni wazi kwamba kutotekeleza ahadi na majukumu yanayohusiana na makubaliano hayo kuna athari hasi kwa pande husika. Ni kama ilivyokuwa kwa pande za Ulaya na Marekani katika JCPOA, ambazo zilipoacha kutekeleza majukumu yaliyobainishwa wazi katika makubaliano ya nyuklia ziliisababishia Iran matatizo kadha wa kadha ya kiuchumi, hatua ya Iran ya kujibu mapigo dhidi ya hatua hiyo, nayo pia haijazifurahisha pande hizo.

Kwa kufuata sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge, likiwa ni jibu kwa kitendo cha upande wa pili katika JCPOA cha kutotekeleza ahadi na majukumu yake, kuanzia tarehe 23 Februari, serikali ya Iran ilisitisha utekelezaji wa hiari wa Protokali ya Ziada ya NPT; na kutokana na hatua hiyo ushrikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki utaendelea kufanyika kulingana na taratibu za kawaida tu za ukaguzi wa shughuli zake za nyuklia.

Bunge la Iran

Wakati huohuo, maafikiano ya karibuni kati ya Iran na IAEA yaliyofikiwa sambamba na kusimamishwa utekelezaji wa hiari wa Protokali ya Ziada, yameanzisha utaratibu mwingine mpya wa ushirikiano kati ya pande mbili utakaotumika kwa muda wa miezi mitatu, jambo linaloonyesha nia njema ya Iran katika kuamiliana na jamii ya kimataifa. Sisitizo la Iran la kuendesha shughuli zake za nyuklia kwa malengo ya amani na kutilia mkazo kwamba itaendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni ithbati ya muelekeo chanya ilionao Tehran kulinganisha na hatua hasi na haribifu za upande wa pili katika makubaliano hayo.

Pande zingine husika katika JCPOA zimepewa fursa nyingine ya muda wa miezi mitatu ya kutekeleza ahadi na majukumu yao na kuondoa vikwazo, ili Iran iweze kunufaika kiuchumi kama ilivyoafikiwa katika makubaliano hayo ya nyuklia. Iran ina msimamo thabiti katika kulinda haki na maslahi yake; na misimamo isiyo ya kimantiki ya pande za Magharibi katika JCPOA haiwezi kuathiri chochote katika misimamo na uchukuaji maamuzi wa Tehran.

Kuhusiana na nukta hiyo, Ismail Baqaee Hamaneh, mwakilishi wa Iran katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, jana Jumatano alitoa jibu kwa matamshi yasiyo ya kimantiki ya maafisa wa nchi za Magharibi waliodai kwamba msimamo wa Iran wa kusitisha utekeleza wa Protokali ya Ziada haujengi bali unaharibu. Hamaneh alisema: Iran itarudi tena kutekeleza majukumu yake katika JCPOA ikiwa tu Marekani, ambayo ndiyo mkosa na mkiukaji wa makubaliano ya nyuklia, itachukua hatua za kivitendo za kurekebisha na kusahihisha makosa yake.

Msingi wa sera za nje za Iran haufuati misimamo ya nchi za Magharibi. Ifahamike wazi kuwa Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia haki na maslahi yake katika uga wa kimataifa kwa kuzingatia misingi mitatu mikuu ya "Heshima, Hekima na Maslahi". Hivi sasa makubaliano mapya yaliyofikiwa baina ya Iran na IAEA yametoa fursa nzuri kwa pande za Ulaya na Marekani ya kutekeleza kivitendo ahadi na majukumu yao katika JCPOA, hususan ya kuondoa vikwazo ili kuandaa mazingira kwa Iran nayo kutekeleza  tena ahadi na majukumu yake katika makubaliano hayo ya nyuklia.

Kuhusiana na suala hilo, Shahryar Heydari, naibu mkuu wa kamati ya bunge ya usalama wa taifa na sera za nje, alisisitiza katika mahojiano aliyofanya jana na shirika la habari la Iran Press ya kwamba, makubaliano ya Iran na IAEA yametoa fursa nzuri kwa nchi za Ulaya na Marekani; na endapo zitatekeleza majukumu yao, ushirikiano wa Iran na wakala huo wa kimataifa wa nishati ya atomiki katika utekelezaji wa Protokali ya Ziada utaendelea tena.

Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA inapasa yaidhaminie Iran maslahi yake; na ikiwa pande nyingine katika makubaliano hayo zitatekeleza majukumu yao, hatua zote mpya ilizochukua Iran katika kadhia ya nyuklia zitarejeshwa kwenye mkondo wake wa awali; lakini kama pande za Magharibi zitaendelea kuchukua misimamo isiyo ya kimantiki, serikali na bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zitaendelea na msimamo wao thabiti na wa pamoja wa kutekeleza kikamilifu sheria ya vipengele tisa ya Hatua ya Kistratejia ya Kuondoa Vikwazo; na wala muelekeo wowote wa kisiasa wa upande wa pili hautaweza kukwamisha suala hilo.../

 

Tags