Iran: Hakuna mazungumo yanayohitajika kwa Marekani kurejea katika JCPOA
(last modified Fri, 12 Mar 2021 02:41:36 GMT )
Mar 12, 2021 02:41 UTC
  • Iran: Hakuna mazungumo yanayohitajika kwa Marekani kurejea katika JCPOA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema mpango wa Marekani wa kutaka kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hauhitaji mazungumzo yoyote kwani Washington haikufanya mazungumzo wala mashauriano na yeyote wakati wa kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa.

Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik la Russia na kuongeza kuwa, iwapo Marekani italiondolea taifa la Iran vikwazo vya kidhalimu na irejee katika JCPOA, hakuna shaka kuwa Tehran nayo itarejea katika majukumu na uwajibikaji wake kama ilivyokuwa huko nyuma.

Ameeleza bayana kuwa, makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA hayana maana wala umuhimu wowote iwapo vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu havitaondolewa.

Amebainisha  kuwa, kitendo cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran cha kupunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo ni radimali kwa hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano hayo kinyume cha sheria.

Vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesisitiza kuwa, jambo la muhimu kwa taifa la Iran ni iwapo kurejea huko kwa US katika JCPOA kutapelekea kufutwa vikwazo hivyo vya kidhalimu au la.

Sayyid Araqchi amebainisha kuwa, miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa matakwa na mahitaji ya taifa hili, na wala haina mfungamano wowote na sera za Marekani katika nchi nyingine za duniani ikiwemo Syria.

 

Tags