Larijani: Iran kuishtaki Marekani ICC kwa kuiba mabilioni ya dola zake
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amekosoa hatua ya Marekani kuzuia dola bilioni 2 za nchi hii katika benki zake na kusisitiza kuwa kadhia hiyo haitasha hivi hivi bila kupata jibu.
Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran ameitaka Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la nchi kuifikisha kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Akiashiria jeuri na kiburi cha Marekani, Larijani ametaja hatua hiyo ya Marekani kama wizi na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Hivi karibuni, Hassan Rouhani Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani wa kuzuia dola bilioni mbili za Iran ni wizi wa wazi na fedheha ya kisheria kwa Marekani na maana yake ni kuendeleza uhasama na uadui dhidi ya Iran.
Ikumbukwe kuwa tarehe 20 Aprili, Mahakama Kuu ya Marekani ilipitisha uamuzi kuwa, katika kuchunguza madai ya waathirika wa eti makosa ya jinai za ugaidi mahakama za nchi hiyo zinaweza kutumia mali na fedha za Iran zilizozuiliwa nchini humo ili kuwalipa fidia watu hao. Mahakama hiyo ilisema dola bilioni mbili za Iran zilizo katika benki za Marekani zipewe familia za wanajeshi wa Marekani waliouawa mwaka 1983 katika hujuma ya bomu huko Beirut Lebanon ambayo Iran inatuhumiwa kuhisika nayo. Iran imekana vikali kuhusika na hujuma hiyo na kusema fedha ambazo mahakama ya Marekani imezichukua ni mali ya Benki Kuu ya Iran.