Iran: Marekani ni mvamizi Syria, itoke haraka
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, madola vamizi ikiwemo Marekani yanapaswa kutoka katika ardhi ya Syria na hiyo ndiyo njia pekee ya kukomesha mapigano nchini humo na kutatuliwa kwa njia za amani mgogoro wa nchi hiyo.
Majid Takh-Ravanchi amesema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili kadhia ya Syria na kuongeza kuwa, mgogoro wa nchi hiyo hautoweza kutatuliwa bila ya kudhaminiwa kwanza haki kamili ya kujitawala ardhi yote ya Syria.
Amesema, si wananchi wa Syria tu ambao hawako tayari kuona nchi yao inaendelea kukaliwa kwa mabavu, lakini jamii ya kimataifa pia hairidhishwi na jambo hilo kwani linakinzana kikamilifu na misingi muhimu zaidi ya haki za kimataifa.
Mwakilishi huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyataka madola yaliyoivamia Syria kinyume cha sheria yatoke haraka katika nchi hiyo, yaheshimu sheria za kimataifa na yaruhusu mchakato wa kutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za amani uendelee inavyopasa.
Takh-Ravanchi amelaani pia wizi wa mafuta ya Syria unaofanywa na dola vamizi la Marekani na pia shambulizi la hivi karibuni lililofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani katika mpaka wa Iraq na Syria na kusema kuwa, vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria vinazidisha tu hali ya wasiwasi na ya mgogoro katika eneo hilo hasa kwa wananchi wa Iraq na Syria.