Mar 17, 2021 07:33 UTC
  • Iran yaadhimisha kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Imam Hussein (AS)

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeungana na ulimwengu wa Kiislamu hii leo kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume wetu mtukufu Muhammad (SAW).

Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo yaani tarehe 3 Shaaban miaka 1438 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (AS) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (AS) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu.

Imam Hussein (AS) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (AS) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (AS), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari.

Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa.

Imam Hussein (AS) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake yaani Imam Hassan bin Ali bin Abi Talib (AS). Hatimaye Imam Hussein (AS) aliuawa shahidi huko Karbala, Iraq mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu.

Radio Tehran inatoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba huu mtukufu wa kukumbuka siku aliyozaliwa Imam Hussein AS. 

Tags