Iran: IAEA imethibitisha kuwa nchi hii inatekeleza JCPOA
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Wakala wa Kimataifa wa Niashati ya Atomiki IAEA kwa mara nyingine tena umethibitisha kuwa Tehran inatekeleza makubaliano ya nyuklia yaliyopewa jina la Utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Katika mazungumzo na Markus Ederer, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani ambaye yuko ziarani hapa nchini, Majid Takht Ravanchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran anayesimamia maswala ya Marekani na Ulaya amesema kuwa Iran inatekeleza barabara makubaliano hayo ya Vienna na kutoa wito kwa pande husika kutekeleza wajibu wao, yakiwemo maswala ya kibenki na kifedha.
Katika mkutano huo wa jana hapa mjini Tehran, mbali na wawili hao kuzungumzia kadhia ya makubaliano ya nyuklia ya Iran, vile vile walibadilishana mawazo kuhusu umuhimu wa Tehran na Berlin kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga tofauti pamoja na maswala ya kieneo na kimataifa.
Mapema mwezi uliopita wa Aprili, Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA pambizoni mwa Kongamano la Usalama wa Nyuklia mjini Washington baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa China, Russia, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya kuhusiana na iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekengeuka mkondo wa miradi ya nyuklia kwa mujibu wa miongozo ya Utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) au la, alisema kuwa, Iran si tu imetekeleza wajibu wake na kuheshimu makubaliano ya Vienna, bali pia imeonyesha uwazi wa hali ya juu wa kukaguliwa vituo vyake vya nyuklia, sambamba na Makubaliano ya Kuzuia Utengenezaji na Usambazaji Silaha za Nyuklia NPT.