Iran yalaani shambulio la kigaidi lililoua 30 Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69926-iran_yalaani_shambulio_la_kigaidi_lililoua_30_afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililoa makumi ya watu katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
(last modified 2026-02-17T02:26:49+00:00 )
May 09, 2021 03:08 UTC
  • Iran yalaani shambulio la kigaidi lililoua 30 Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililoa makumi ya watu katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Saeed Khatibzadeh amekosoa vikali hujuma hiyo ya kigaidi iliyolenga raia wa kawaida hususan wanafunzi na wanachuo. Kadhalika ametoa mkono wa pole kwa jamaa za waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo la jana Jumamosi.

Tariq Arian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afghanistan amesema watu zaidi ya 30 aghalabu yao wakiwa ni wanafunzi wa kike wenye umri kati ya miaka 11 na 15 wameuawa, baada ya kujiri mripuko karibu na shule ya Syed Al-Shahda, katika wilaya ya Dasht-e-Barchi iliyoko magharibi mwa Kabul.

Aghalabu ya wakazi wa eneo hilo ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Naye Ghulam Dastagir Nazari, msemaji wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo amesema watu zaidi ya 50 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.

Wasamaria wema wakibeba miili ya waliouawa katika hujuma ya kigaidi

Wakati huohuo, Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan amelaumu kundi la Taliban kuwa limetekeleza hujuma hiyo, ingawaje kundi hilo linasisitiza kuwa halijahusika. Kundi hilo limetoa taarifa ya kulaani hujuma hiyo.

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya watu zaidi ya 30 kuuawa katika hujuma nyingine ya kigaidi katika eneo la Puli-e-Alam, jimbo la Logar nchini Afghanistan.