May 13, 2021 08:10 UTC
  • Swala ya Idi, Iran
    Swala ya Idi, Iran

Maelfu ya Waislamu wa Iran leo wameshiriki katika Swala ya Idul Fitri kwa kuchunga sheria na taratibu za kuzuia maambukizi ya corona, baada ya kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Maelfu ya waumini tangu mapema leo walielekea kwenye misikiti, Haramu tukufu na maeneo mengine ya ibada kwa ajili ya Swala ya Idi wakimshukuru Mwenyezi Mungu SW kwa kuwapa taufiki ya kutekeleza faradhi wa Swaumu na kufunga mwezi wa Ramadhani.

Katika miji yenye idadi kubwa ya maambukizi ya corona, Swala ya Idi imefanyika kwenye maeneo ya wazi na nje ya misikiti na majengo ya ibada. 

Mjini Tehran, Swala ya Idul Fitri imeongozwa na Hujjatul Islam Walmuslimin Mustafa Rostami ambaye ni mkuu wa Ofisi ya Mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu. Swala hiyo ya Idi imefanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran ili kulinda sheria na desturia za kuzuia maambukizi ya corona.

Kwa mnasaba wa sikukuu hii ya leo Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia ujumbe viongozi wa nchi za Waislamu akiwapa mkono wa heri na baraka na kusema ana matarajio kwamba, viongozi hao watafanya jitihada kubwa zaidi za kuimarisha mahusiano na udugu katika Umma wa Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani

Rais Rouhani amesema sikukuu ya Idi ni sherehe ya kurejea katika maumbile safi na asili ya mwanadamu na msimu wa furaha wa watu waliokuwa kwenye ibada ya Swaumu na waja wa Mwenyezi Mungu ambao wamefanikiwa kuosha na kusafisha roho zao kwenye mto wenye maji safi wa Ramadhani.

Amesema ana matarajio kwamba, kwa baraka za sikukuu hii adhimu, Umma wa Kiislamu utashuhudia kudhubitiwa na kuzuia kabisa janga la maradhi ya Covid-19 katika maeneo yote ya dunia.

Leo Akhamisi imetangazwa kuwa ni sikukuu ya Idul Fitri katika nchi nyingi za Kiislamu. 

Tags