Apr 10, 2024 03:38 UTC
  • Jumatano, tarehe 10 Aprili, 2024

Leo ni tarehe Mosi Shawwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 2024.

Tarehe Mosi Shawwal inayosadifiana na sikukuu ya Idul Fitr.

Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo.

Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Sala ya Iddul Fitr.

Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi, yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani. *

Siku kama ya leo miaka 1192 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253, Hijria alifariki dunia mpokezi mashuhuri wa Hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari.

Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta Hadithi za Mtume (saw).

Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha ‘Jamius Swahih’ maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni ‘Al-Adabul Mufrad’, ‘Al-Jaamiul-Kabiir’ na ‘Tarikhul-Kabir an Taraajam Rijaal-Sanad.’

Muhammad Ismail Bukhari

Siku kama ya leo miaka 876 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Shawwal mwaka 569 Hijiria alifariki dunia Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu.

Ibn Dahhan alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake.

Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi. Aidha alilipa umuhimu mkubwa suala la kuhuisha baadhi ya vitabu vilivyosahaulika kiasi kwamba mwishoni alipoteza uwezo wake wa kuona katika kazi hiyo.

Miaka 839 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe Mosi Shawwal alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu.

Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama Fiqihi, Tafsiri, Falsafa na Mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho.

Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya Fakhrurazi ni Sherh Nahaj al-Balagha, Nihayat al-Uquul wa Siraj al-Quluub.

Fakhrurazi

Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, alifariki dunia Joseph-Louis Lagrange, mwanahisabati maarufu wa Ufaransa. Lagrange alizaliwa mwaka 1736 Miladia huko mjini Turin, Italia. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Uchunguzi wa Umekanika' ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 25.

Joseph-Louis Lagrange

Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, aliuawa Emiliano Zapata mwanamapinduzi mashuhuri wa nchini Mexico kupitia njama maalumu dhidi yake. Wahindi Wekundu wa Mexico wanamfahamu Zapata kama mrekebishaji wa jamii na mwokozi wao. Tangu mwishoni mwa mwaka 1910 Miladia sanjari na kutoa nara za kupigania uhuru, alibeba pia silaha na kuwaongoza Wahindi Wekundu katika kupambana na wavamizi na kufanikiwa kuzikomboa ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa. 

Emiliano Zapata

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 1946, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka huko Lebanon.

Ufaransa ilizikalia kwa mabavu Lebanon na Syria wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Lebanon ilipata uhuru mwaka 1945 na mwaka huo huo ikatia saini makubaliano ya kuondoka askari wa Uingereza na Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo ambayo yalianza kutekelezwa Aprili 1946. 

Beirut, Lebanon

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita yaani sawa na tarehe 10 Aprili 1973, makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD waliwaua maafisa watatu wa Palestina huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon.

Katika kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina, miaka kumi baadaye utawala wa Kizayuni wa Israel yaani tarehe 10 Aprili 1983, ulimuuwa huko Ureno, Isam Sartawi aliyekuwa mshauri wa Yassir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO).

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa ajili ya kuendelea kujipanua na kuzima mapambano ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Isam Sartawi

Na katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran.

Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekuwa akiishi Ujerumani. Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Takribani miezi kumi baadaye mabalozi wa Umoja wa Ulaya walianza kurejea hapa Tehran mmoja baada ya mwingine. 

 

Tags