Takht-Ravanchi: Himaya kwa makundi ya kigaidi nchini Syria inapaswa kukomeshwa
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuna ulazima wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kusisitiza kuwa: Lazima tukomeshe kuwagawa magaidi baina ya magaidi wazuri na magaidi wabaya.
Majid Takht-Ravanchi alisema hayo jana kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana kujadili masuala ya kisisa ya Syria.
Amesema, Iran inafanya jitihada za kutatua mgogoro wa Syria kwa njia za amani na inaamini kuwa, sambamba na jitihada za kuitishwa kikao kijacho cha Kamati ya Katiba ya Syria, kuna udharura wa kuwepo hatua athirifu za kudhamini umoja wa ardhi yote ya Syria na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuhitimishwa kuikalia kwa mabavu Syria na kuondoka majeshi yote ya kigeni ambayo hayajaalikwa na serikali ya Damascus katika ardhi ya nchi hiyo na amepinga harakati yoyote inayotaka kugawanywa nchi hiyo na kukanyaga mamlaka yake ya kujitawala hususan utawala haramu wa Israel. Amesema Iran inalaani vitendo na harakati kama hizo.
Amesema kuwa himaya na uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi katika baadhi ya ardhi za Syria vinapaswa kukomeshwa na vilevile kuna ulazima wa kusimamishwa jitihada za kuyaarifisha baadhi ya makundi ya kigaidi kuwa ni magaidi wenye misimamo ya wastani au kutaka kuwagawa magaidi baina ya magaidi wazuri na magaidi wabaya.
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia ametoa wito wa kuhitimishwa mashaka na matatizo ya raia wa Syria na kusema: Katika uwanja huo Umoja wa Mataifa unapaswa kuchukua hatua zitakazopunguza mashaka ya watu wa Syria haraka iwezekanavyo na kuwarejesha wakimbizi wa ndani katika makazi yao.
Vilevile ameshutumu vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Syria akivitaja kuwa si vya kuwajibika na vinakiuka maadini na kuongeza kuwa: Iran inalaani hatua yoyote ya kutumia chakula na dawa kama silaha.