Jun 09, 2021 12:41 UTC
  • Mgombea urais Iran aahidi kutumia vizuri fursa za kiuchumi za Afrika iwapo atachaguliwa

Mgombea mmoja katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, iwapo atachaguliwa, serikali yake itatumia vizuri sana uwezo wa kila namna wa kiuchumi wa nchi za Afrika katika ustawi wa pande mbili na pande kadhaa.

Mohsen Rezaee amesema hayo baada ya kumalizika mdahalo wa pili wa wagombea urais nchini Iran na kujibu swali aliloulizwa na mwandishi wa Iran Press kwamba atatumia vipi fursa nyingi na za kila namna za kiuchumi za barani Afrika akisema, serikali yake itakuwa na ratiba nzuri za uwekezaji na ushirikiano na nchi za Afrika hasa katika sekta za madini na kilimo.

Vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahitajia eneo kubwa zaidi la ardhi na maji kuweza kuzalisha chakula cha milioni 500.

Amesema, bara la Afrika lina neema ya ardhi na maji na kwa sasa hivi baada ya Marekani na Ulaya, Wairani wengi wako katika nchi za Afrika. Amesema hivi sasa takriban raia laki tano wa Iran wanaishi barani Afrika.

Mdahalo wa pili wa uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

 

Mohsen Rezaee pia amesema, uhusiano mkubwa wa kihistoria baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Afrika na uhusiano mkubwa na wa muda mrefu wa kiutamaduni na kiustaarabu baina ya Iran na nchi za Afrika, utatumiwa vizuri na serikali yake kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili na pande kadhaa kadiri itakavyowezekana.

Mdahalo wa pili wa wagombea saba wa urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanyika Jumanne jioni na mada yake ilikuwa ni "Utamaduni, Jamii na Siasa." Mdahalo huo ulirushwa hewani mubashara na Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 18 mwezi huu wa Juni, 2021.

Tags