Iran haitasalimu amri mbele ya ubabe wa Marekani
Kamanda mwandamizi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu kamwe haiwezi kulegeza misimamo au kusalimu amri mbele ya vitendo vya ubabe wa Marekani katika eneo.
Naibu Mkuu wa Majeshi ya Iran Brigedia Jenerali Massoud Jazayeri amesema Marekani imezoea kueneza ubabe dhidi ya nchi zingine duniani na inataraji nchi hizo zikae kimya mbele ya hujuma hizo.
Ameongeza kuwa Iran ilionyesha mwenenedo wa amani wakati askari 10 mabaharia wa Marekani walipoingia katika maji ya Iran kinyume cha sheria mwezi Januari. Brigedia Jenerali Jazayeri amesema ingawa askari hao wa Marekani walikuwa wavamizi na Iran ikawasamehe, lakini serikali ya Marekani haijaonyesha nia njema kuhusu hatua hiyo ya amani ya Iran. Amesema hivi sasa kuna ishara kuwa Marekani ilighadhibishwa na kukamatwa askari wake katika maji ya Iran ya Ghuba ya Uajemi.
Kwingineko Brigedia Jenerali Hussein Salami Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema, utamaduni wa kujihami Iran umejengeka katika misingi ya subira, mapambano, ukakamavu na kujiamini.
Akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Utamaduni wa Kujihami, Brigedia Salami amesema mataifa ambayo yamefungamanisha fikra na mitazamo yao na fikra na mitazamo ya madola ya kibeberu huwa hayana fikra huru na hivyo humezwa na tamaduni hizo za mabeberu na kwa msingi huo hukosa uhai halisi wa kibinadamu katika maisha. Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema moja ya alama za uhai wa taifa ni uhuru na kujitegemea kwake katika sekta zote na kwamba utamaduni ni nembo asili ya utambulisho wa kila taifa.