Jun 18, 2021 02:17 UTC
  • Mohammad Bagher Ghalibaf
    Mohammad Bagher Ghalibaf

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesisitiza kuwa, matatizo ya nchi hayawezi kutatuliwa kwa kususia uchaguzi, bali jukumu kuu la wapiga kura ni kushiriki kwa wingi katika uchaguzi na kumchagua mtu ambaye wanaamini atawatatulia matatizo yao.

Mohammad Bagher Ghalibaf alisema hayo jana wakati akitembelea mji wa Pardis ulioko kwenye viunga vya mji mkuu wa Iran, Tehran na kusema akiwa katika msikiti wa Imam Ali AS wa mji huo kwamba, wanaochochea watu wasishiriki katika uchaguzi ni maadui tu wa taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu ambao lengo lao hasa ni kuupindua mfumo wa Kiislamu unaotawala humu nchini.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeanza mapema leo Ijumaa, ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, mapema kabisa leo asubuhi ameshiriki kutumia haki yake ya kupiga kura.

Uchaguzi

 

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake ya jana, Ghalibaf amesema, wananchi wanapaswa kuwapigia kura watu ambao watasikiliza vilio vyao na watailetea mustakbali mzuri nchi. 

Spika huyo wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, Mapinduzi ya Kiislamu na Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu imewapa wananchi uhuru kamili wa kujiamulia mambo yao. Miongoni mwa uhuru na haki hiyo ni uchaguzi ambapo katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wananchi wamepewa pia haki yao ya kuchagua Rais ambaye ataiongoza nchi kwa muda wa miaka minne ijayo.

Tags