Spika wa Bunge la Iran: AEOI haitaikabidhi IAEA video za taarifa zake
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI) halitaukabidhi Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) video zilizonakili taarifa za taasisi hiyo ya Iran, kwa kuwa muhula uliokuwa umeainishwa umemalizika, wala haujarefushwa tena.
Muhammad Qalibaf amesema hayo leo Jumapili akijibu suali la Mbunge Alireza Salimi, katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran na kufafanua kuwa: Muda uliokuwa umeanishwa umemalizika siku tatu zilizopita na kwa msingi huo Iran haitaipa IAEA taarifa zozote zilizonakiliwa na kamera za CCTV za wakala huo hapa nchini.
Mbunge huo alitaka kujua msimamo wa Bunge la Iran juu ya sheria ya "Hatua ya Kistratejia ya Kuondoa Vikwazo na Kulinda Haki za Taifa la Iran" na hatua ya Iran ya kusimamisha utekelezaji wa hiari wa Protokali ya Ziada, baada ya upande wa pili wa mapatano ya JCPOA kutochukua hatua zozote za maana za kuliondolea taifa hili vikwazo.
Spika Qalibaf amemjibu mbunge huyo wa Iran kwa kubainisha kuwa, "Tayari nimezungumza juu ya wakala huo, na sasa nasema kuwa, baada ya muda wa muhula wa miezi mitatu iliyotolewa kumalizika, muhula huo haujarefushwa tena, na kwa msingi huo, hakuna taarifa yoyote iliyorekodiwa hapa nchini itakabidhiwa wakala huo (IAEA), na rekodi zote zipo mikononi mwa Jamhuri ya Kiislamu."
Februari mwaka huu, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI) alisema kuhusu mapatano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Iran na IAEA kwamba, kwa muda wa miezi mitatu, wakala huo hautakuwa na haki ya kuangalia kamera na mifumo ya kurekodia taarifa; na kama vikwazo havitaondolewa katika miezi mitatu ijayo, taarifa hizo zitafutwa na kamera za wakala huo wa nishati ya atomiki zitaondolewa.
Muhula huo ulimalizika mwezi Mei, na Jamhuri ya Kiislamu ikaenda mbali zaidi kwa kuurefusha kwa kipindi cha mwezi mwingine mmoja, ili kuupa fursa upande wa pili wa mapatano hayo ya nyuklia kuyanusuru kwa kuwaondolewa wananchi wa Iran vikwazo vya kidhalimu.
Hata hivyo mazungumzo ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, yanaonekana kusuasua. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema haitajihusisha na mazungumzo yasiyo na kikomo.