Waziri Mkuu wa Pakistan azungumza kwa simu na Rais mteule wa Iran
Waziri Mkuu wa Pakistan, amefanya mazungumzo ya simu na Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ikulu ya Pakistan imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Imran Khan amefanya mazungumzo ya simu na Sayyid Ibrahim Raisi, Rais mteule wa Iran na huku akimpongeza kwa kuchaguliwa kuliongoza taifa la Iran ameelezea matumaini yake kuwa, karibuni hivi watapata nafasi ya kuonana ana kwa ana.
Waziri Mkuu wa Pakistan amegusia masuala mengi muhimu yanayoziunganisha nchini hizi mbili ndugu jirani za Kiislamu na kuongeza kuwa, Pakistan nayo ina wasiwasi mkubwa na hali ya Afghanistan na hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu nchini humo.

Amesema, njia bora kabisa ya kutatua mgogoro wa Afghanistan ni mazungumzo ya kisiasa ingawa suala hilo hivi sasa ni zito sana kulifikia.
Kwa upande wake, Sayyid Ibrahim Raisi, Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemshukuru Waziri Mkuu wa Pakistan kwa kumpigia simu na kusema kuwa, ujumbe wa pongezi uliotolewa na taifa na serikali ya Pakistan unaonesha jinsi mataifa haya mawaili ya Kiislamu yalivyo na udugu ulioimarika katika kila upande na hiyo ni fursa nzuri ya kustawishwa zaidi na zaidi ushirikiano wa pande mbili katika nyuga zote.
Vile vile amesema, mafanikio ya serikali rafiki na taifa ndugu la Pakistan ni mafanikio ya serikali na taifa la Iran na kusisitiza kuwa, kuaminiana na kushirikiana nchi za ukanda huu ni masuala mawili muhimu sana ya kuimarishwa utulivu na usalama katika eneo hili.