Iran na Algeria zasaini hati 19 za maelewano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i7294-iran_na_algeria_zasaini_hati_19_za_maelewano
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Algeria zimesaini hati 19 za maelewano mwishoni mwa kikao cha pili cha kamati ya pamoja ya kutathmini ushirikiano wa kiviwanda baina ya nchi mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 18, 2016 03:26 UTC
  • Iran na Algeria zasaini hati 19 za maelewano

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Algeria zimesaini hati 19 za maelewano mwishoni mwa kikao cha pili cha kamati ya pamoja ya kutathmini ushirikiano wa kiviwanda baina ya nchi mbili.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika hapa mjini Tehran, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran Mohammad Reza Neematzadeh amesema kusainiwa hati hizo za maelewano kunadhihirisha ushiriki chanya wa Algeria nchini Iran kwa ajili ya kustawisha ushirikiano.

Neematzadeh ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Algeria zina utajiri mkubwa wa maliasili za mafuta na gesi, hivyo nchi hizo mbili zinapaswa kuzitumia rasilimali hizo kwa ajili ya ustawi wa kiviwanda na kiuchumi.

Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran amebainisha kuwa Iran ina uwezo mzuri katika nyuga za usanifu na uhandisi, utengenezaji zana mbalimbali, ujenzi wa viwanda vya kusafisha mafuta na vya petrokemikali na iko tayari kuipatia uzoefu wake nchi rafiki ya Algeria katika nyuga hizo bila ya gharama yoyote.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Madini wa Algeria Abdesalam Bouchouareb amesema, sasa ni wakati wa Iran kuwepo nchini Algeria na kuongeza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko katika nafasi nzuri kiviwanda kati ya nchi kubwa duniani.../