Wingu la huzuni na majonzi latanda Iran katika maombolezo ya Ashura
(last modified Thu, 19 Aug 2021 08:02:54 GMT )
Aug 19, 2021 08:02 UTC
  • Wingu la huzuni na majonzi latanda Iran katika maombolezo ya Ashura

Wananchi Waislamu waombolezaji hapa Iran leo wanashiriki kwenye vikao vya maombolezo kukumbuka ushujaa na dhulma waliotendewa mashahidi wa Karbala kkwa mnasaba wa siku ya Ashura.

Wananchi wa matabaka tofauti ya Iran wakiwemo vijana na wazee, wake kwa waume wanashiriki kwenye maombolezo hayo ya kukumbuka siku aliyouliwa shahidi Imam Hussein AS pamoja na masahaba zake 72 katika jangwa la Karbala.

Harakati za waombolezaji wanaobubujikwa na machozi kwa majonzi na huzuni kwa dhulma iliyofanywa na wana wa shetani dhidi ya kizazi bora cha wanadamu, huku wakipaza sauti zao kupinga madhila na udhalili, zimezijaza hamasa na msisimko mkubwa majlisi za maombolezo ya Siku ya Ashura katika kila pembe ya Iran ya Kiislamu.

Kutokana na maombolezo ya mwaka huu kufanyika katika mazingira ya maambukizi ya virusi vya corona, waombolezaji wanashiriki katika majlisi za Ashura zinazofanyika katika maeneo ya wazi kwa nidhamu maalumu inayozingatia na kuchunga kikamilifu miongozo ya kiafya.

Waombolezaji wakishiriki katika majlisi za Muharram kwa kuzingatia na kuchunga miongozo ya kiafya

 

Katika tukio la Karbala lililojiri katika siku kama ya leo mnamo mwaka 61 Hijria, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, Imamu wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani alisisitiza na kueleza bayana kwamba: "Kusudio langu ni kuufichua na kuufedhehesha utawala ulio dhidi ya Uislamu, kuamrisha mema na kukataza mabaya na kukabiliana na dhulma na uonevu."

Mafunzo ya harakati ya Imam Hussein AS yamesambaa na kutanda katika historia na jiografia ya viumbe, wanadamu na ulimwengu mzima na hayawezi katu kuishia kwenye mipaka maalumu.