Iran yatilia mkazo wajibu wa kulindwa usalama na utulivu nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74450-iran_yatilia_mkazo_wajibu_wa_kulindwa_usalama_na_utulivu_nchini_afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, suala la usalama na utulivu wa Afghanistan ni muhimu sana kwa Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 09, 2021 07:35 UTC
  • Iran yatilia mkazo wajibu wa kulindwa usalama na utulivu nchini Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, suala la usalama na utulivu wa Afghanistan ni muhimu sana kwa Iran.

Hossein Amir-Abdollahian ameandika hayo na kuongeza kuwa, suala la usalama, utulivu na ustawi wa Afghanistan limejadiliwa pia katika kikao kilichofanyika kwa njia ya Intaneti, cha nchi sita zinazopakana na nchi hiyo. 

Aidha ameandika: Katika kikao hicho, kulihimizwa kuundwa serikali kubwa ya watu wa matabaka yote itakayoridhiwa na jamii ya Waafghani, kutilia mkazo mazungumzo na kujiweka mbali na machafuko, utumiaji nguvu na uingiliaji wa kigeni.

Kikao cha nchi sita zinazopakana na Afghanistan kilifanyika kwa njia ya Intaneti jana Jumatano. Nchi zilizoshiriki kwenye kikao hicho ni Iran, China, Pakistan, Uzbekistan, Tajikistan na Turkmenistan. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Imarati,  Hossein Amir-Abdollahian (kulia) na Abdullah bin Zayed Al Nahyan

 

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed Al Nahyan, usiku wa kuamkia leo amefanya mazungumzo ya simu na Bw. Hossein Amir-Abdollahian. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pande hizo mbili zimetilia mkazo wajibu wa kuimarishwa uhusiano wao zikiwa ni nchi jirani ambazo kila moja inamuhitajia mwenzake, kama ambavyo zimejadiliana pia masuala ya kieneo na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Bw. Abdollahian amegusia mazungumzo yake ya hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed bin Rashid Al Maktoum na jinsi pande mbili zilivyo na mitazamo chanya kuhusu ushirikiano baina yao katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ustawi.