Amir Abdollahian: Marekani ndio chanzo cha kuvurugika uthabiti Afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Marekani imechangia pakubwa katika kuvurugika amani na uthabiti nchini Afghanistan.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwenye kikao cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa anuani ya "hali ya huduma za kibinadamu nchini Afghanistan".
Katika kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya intaneti chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Amir-Abdollahian amesema: "sisi sote leo tunakabiliana na mazingira mapya na changamoto mpya nchini Afghanistan na tunaamini kuwa lililochangia pakubwa kuvurugika uthabiti, usalama na kuwepo hali ya mchafukoge ya hivi sasa nchini Afghanistan ni sera za kujaribu na kubahatisha za Marekani katika nchi hiyo."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa, Marekani imesababisha majanga na maafa nchini Afghanistan katika miaka ya uvamizi na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo na hivi sasa pia kwa namna ilivyoondoka katika nchi hiyo, ambapo walimwengu wameshuhudia hali hiyo mnamo siku zilizopita katika uwanja wa ndege wa Kabul na akafafanua kuhusu ujumbe wa kikao hicho kwa mtazamo wa kisiasa na kiutu kwa kusema: Katika upeo wa kisiasa, inapasa tufikishe ujumbe mmoja kwa Afghanistan wa kwamba Afghanistan yenye amani, uthabiti na ustawi itaweza kujengwa kwa njia moja tu, ambayo si nyingine isipokuwa kuundwa serikali jumuishi ya kitaifa itakayoshirikisha pande zote.
Kwa upande wa kiutu, Abdollahian amebainisha mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusema: tunaitakidi kuwa kwa upande wa huduma za kibinadamu, katika miaka iliyopita na katika wiki za karibuni, wananchi, wanawake na watoto wa Afghanistan wamekabiliiwa na hali mbaya na ya kusikitiisha na leo hii jamii ya kimataifa ina wajibu na inapaswa kupeleka haraka sana misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa Tehran inawasiliana na pande zote nchini Afghanistan na akongeza kwamba: mbali na suala la kuundwa serikali pana na jumuishi, sera zinazofuatiliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afghanistan ni kuhakikisha nchi hiyo inasafika na ugaidi na madawa ya kulevya; na wananchi wenyewe wa Afghanistan wanakuwa na uwezo wa kuamuua juu ya mustakabali na hatima ya nchi yao.../