Iran: Hakuna dola lolote linalothubutu kuishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu
Mshauri Mkuu wa Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran amesisitiza kuwa, hakuna dola lolote duniani linalothubutu kuishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu.
Shirika la habari la Mehr limemnukuu Meja Jenerali Sayyid Yahya Rahim Safavi akisema hayo na kuongeza kuwa, wananchi wa Iran na vikosi vyao vya ulinzi wana nguvu kubwa kiasi kwamba hakuna dola lolote la nje ya eneo hili kama vile Marekani na mengineyo lenye uwezo wa kuanzisha chokochoko za kijeshi dhidi ya nguvu hizo za Iran.
Mshauri huyo Mkuu wa Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Iran vile vile amesema, hivi sasa miaka 40 imepita tangu ilipofelishwa operesheni ya kuizingira Abadan, na bado mshikamano mzuri sana ungalipo baina ya Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.
Luteni Jenerali Safavi vile vile amesisitiza kuwa, mshikamano huo madhubuti ulioanzia zama za vita vya miaka minane ya kujihami kutakatifu vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivi sasa umekuwa mkubwa na imara zaidi.
Aidha amesisitiza kuwa, Iran hivi sasa ni taifa nambari moja lenye ushawishi mkubwa katika milingano ya eneo la Asia Magharibi, na nguvu za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye eneo hilo ni kubwa na zenye taathria katika milingano ya kiulinzi na kiusalama.
Luteni Jenerali Rahim Safavi pia amesema, leo hii vikosi vya majini vya Iran vina nguvu kiasi kwamba, msafara wa vyombo vya baharini vya vikosi hivyo vina nguvu za kuvuka bahari kubwa ya Atlas na kufika kwenye bandari ya Saint Petersburg nchini Russia.