Ndege ya misaada ya kibinadamu ya Iran yatua mjini Kabul, Afghanistan
Ndege yenye misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya wananchi wenye shida wa Afghanistan, imetua katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul na misaada hiyo kukabidhiwa viongozi wa serikali ya mpito ya Taliban.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, hiyo ni shehena ya tano ya misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Afghanistan. Imewasili leo asubuhi katika uwanja wa ndege wa Kabul na sherehe za kukabidhiwa viongozi wa serikali ya mpito ya Taliban zimemshirikisha balozi wa Iran mjini humo.
Ubalozi wa Iran mjini Kabul umesema kuwa, shehena hiyo ni ya misaada ya chakula, madawa na vitu vya matibabu na imetumwa nchini Afghanistan na Shirika la Hilal Nyekundu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kukabidhiwa kwa maafisa wa Hilal Nyekundu wa Afghanistan.
Jana Jumatatu pia, shehena ya nne ya misaada ya kibinadamu ya Iran ambayo pia ilikuwa na chakula na madawa iliwasili nchini Afghanistan kupitia mpaka wa nchi kavu na kukabidhiwa maafisa wa serikali ya mpito ya Taliban.
Shehena hiyo ya jana ilikuwa na tani 94 ya bidhaa za mahitaji muhimu ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Afghanistan.
Shehena nyingine tatu za misaada ya kibinadamu ya Iran kwa wananchi wa Afghanistan iliwasili nchini humo wiki zilizopita.
Muda wote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko pamoja na wananchi wa Afghanistan kwa hali na mali na haijawahi kusita kutoa msaada wowote unaohitajika kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 sasa.