Iran: Hatutaruhusu uwepo wa Israel karibu na mipaka yetu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i75632-iran_hatutaruhusu_uwepo_wa_israel_karibu_na_mipaka_yetu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu katu haitaruhusu uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel karibu na mipaka yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2021 04:44 UTC
  • Iran: Hatutaruhusu uwepo wa Israel karibu na mipaka yetu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu katu haitaruhusu uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel karibu na mipaka yake.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, "Ujumbe wa Iran upo wazi kabisa, na imebainika wazi kivitendo kuwa Israel haiwezi kuwa karibu (na mipaka ya Iran)."

Ameashiria uwepo wa Israel mjini Baku na kueleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan hazipaswi kuruhusu mshirika wa tatu kuingilia mambo yao.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unapenda kuliona eneo la Asia Magharibi halina usalama.

Ghuba ya Uajemi

Khatibzadeh amebainisha kuwa, kila sehemu ambayo Israel imetia mguu, hakuna matokeo mengine yaliyoonekana ghairi ya ukosefu wa usalama na uthabiti; sambamba na kushamiri harakati za ugaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Iran inalitazama kwa mazingatio makubwa suala la usalama wa taifa, na majirani wote wa nchi hii wanalifahamu vyema hilo.