Iran na Afrika Kusini zaafikiana kuimarisha ushirikiano wao
Serikali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimeazimia kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za kieneo na kimataifa.
Katika mazungumzo ya simu, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Naledi Pandor wamebadilishana mawazo na kukubaliana kuhusu kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi mbili hizi katika nyuga za kieneo na kimataifa.
Safari inayotazamiwa kufanyika hapo baadaye ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Afrika Kusini ni miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa na mawaziri hao katika mazungumzo yao ya simu.
Wawili hao wamesisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia wa Tehran na Pretoria katika ngazi za mawaziri na manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili hizi.

Bi Pandor amegusia kuhusu mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran pambizoni mwa mkutano uliopita wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kueleza kuwa, kuna haja ya kuboreshwa zaidi uhusiano wa pande mbili.
Amesema safari ijayo ya Sayyid Raisi mjini Pretoria inaashiria namna Afrika Kusini inautazama kwa umuhimu mkubwa uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amir-Abdollahian kwa upande amesema vikao vijavyo vya kamati za pande mbili za Iran na Afrika Kusini vinavyotazamiwa kufanyika ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka ujao, vinapaswa kutoa kipaumbele kwa masuala ya uwekezaji, nishati, afya na ushirikiano wa kimataifa.