Khatibzadeh: Mapatano ya awali yamefikiwa katika mazungumzo ya Iran na Saudia
(last modified Sun, 31 Oct 2021 12:32:05 GMT )
Oct 31, 2021 12:32 UTC
  • Khatibzadeh: Mapatano ya awali yamefikiwa katika mazungumzo ya Iran na Saudia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mapatano ya awali yamefikiwa katika mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia.

Saeed Khatbizadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyadokeza hayo leo katika mazungumzo na Shirika la Habari la Mehr kuhusu hali ya hivi karibuni ya mazungumzo baina ya Iran na Saudia. Ameongeza kuwa, hadi sasa kumefanyika duru nne za mazungumzo na mawasiliano baina ya nchi mbili yanaendelea.

Kuhusu kufunguliwa tena balozi za Iran na Saudi Arabia, Khatibzadeh  mesema hadi hakujafikiwa mapatano ya kufunugliwa balozi za nchi mbili katika miji ya Riyadh na Tehran.

Siku ya Jumamosi  Faisal bin Farhan Al Saud, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia akizungumza mjini Roma Italia pembizoni mwa mkutano wa viongozi wa G20 alisema mazungumzo baina ya Iran na Saudia yamekuwa ya kirafiki lakini bado hakuna mafanikio makubwa hayajapatikana. 

Mnamo mwaka 2016, Saudia ilichukua hatua ya upande mmoja ya kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa kisingizio cha baadhi ya watu kuvamia ofisi zake za kidiplomasia mjini Tehran na Mashhad. Katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita, Iran imetangaza mara kadhaa kuwa iko tayari kufufua uhusiano wake na Saudi Arabia, lakini Riyadh imekuwa ikipiga upatu wa kuendeleza mvutano na Tehran.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, kumekuweko na mazungumzo baina ya Iran na Saudia kwa usimamizi wa Iraq.

Juzi Mkuu wa Shirikisho la Usafirishaji Nje Bidhaa za Iran alisema kuwa, uhusiano wa kiuchumi wa nchi yake na Saudi Arabia umeanza rasmi baada ya meli moja yenye bidhaa za Iran kutia nanga katika moja ya bandari za Saudia.

Mohammad Lahooti aliongeza kuwa, maelewano ya kisiasa yana taathira pia katika ushirikiano wa kiuchumi na kwamba iwapo mivutano itazidi kupungua, basi harakati za kiuchumi na kibiashara nazo zitanawiri.

Tags