Khatibzadeh: Vitisho haviwezi kuzaa matunda mbele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kujibu matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken aliyedai kuwa Washington inatafuta machaguo mengine ya kukabiiana na Iran na ameandika: Vitisho kamwe havijawahi kuzaa matunda mbele ya Iran.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Saeed Khatibzadeh akisena hayo na kuongeza kuwa, machaguo yanayozungumziwa na Marekani si kitu kimpya, yameshafanyiwa majaribio na kufeli katika eneo hili. Kushindwa vibaya na kwa fedheha Marekani katika njama zake dhidi ya nchi za eneo la Asia Magharibi kuko wazi na kila mmoja anakuona.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vile vile amesema kuwa, Marekani ndiye msababishaji mkuu wa matatizo yote yaliyopo hivi sasa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
JCPOA ni makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 kati ya Iran kwa upande mmoja na kundi la 5+1 kwa upande wa pili. Kundi hilo la 5+1 liliundwa na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Utekelezaji rasmi wa makubaliano hayo ulianza mwezi Januari 2016, lakini rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump aliamua kuitoa nchi yake kijeuri kwenye mapatano hayo ya kimataifa, tarehe 8 Mei 2018 na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo. Iran nayo ilichukua hatua mbalimbali za kisheria za kukabiliana na hatua hiyo ya Marekani lakini haikujitoa kwenye mapatano hayo ya JCPOA.
Viongozi wa serikali ya hivi sasa ya Joe Biden huko Marekani mara kwa mara wamekuwa wakikiri kushindwa vikwazo vya kiwango cha juu vilivyowekwa na Trump dhidi ya Iran, lakini pamoja na hayo hawajifunzi kutokana na makosa yao.