Iran: Madola ya Ulaya yanapaswa kuvuka mstari wa Marekani wa kutotekeleza ahadi
(last modified Mon, 07 Feb 2022 12:52:08 GMT )
Feb 07, 2022 12:52 UTC
  • Iran: Madola ya Ulaya yanapaswa kuvuka mstari wa Marekani wa kutotekeleza ahadi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, madola ya Ulaya yanapaswa kuvuka mstari wa Marekani wa kutotekeleza ahadi na kueleza kwamba, Tehran inasubiri kuona mabadiliko kivitendo katika mwenenendo wa Washington.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari wa ndani na wa nje ambapo akizungumzia kuanza tena mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria hapo kesho Jumanne ameeleza kwamba, matarajio ya Iran ni kwamba, timu na jumbe za mazungumzo ukiwemo ujumbe wa Marekani zinarejea katika mazungumzo hayo zikiwa na ajenda za wazi kwa ajili ya kutekeleza kivitendo ahadi zao katika mkondo wa kuliondolea vikwazo taifa hili.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, viongozi wa Marekani wanapaswa kutambua kwamba, maamuzi mabaya, haribu na yasiyo sahihi ukiwemo uamuzi wake wa kujiondoa kinyamela katika makubaliano ya nyuklia yana gharama kubwa na kwamba, hawawezi kulipa gharama hizo kupitia mifuko ya wananchi wa Iran.

 

Akizungumzia matamshi ya Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel kuhusiana na kupatikana maafikiano katika mazungumzo ya Vienna, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wazayuni ni chimbuko la mauaji na umwagaji damu katika maeneo yote ya Asia Magharibi. Khatibzadeh amebainisha kwamba: Marafiki zetu katika eneo wanapaswa kuwa macho na njama za Wazayuni maghasibu.

Kuhusiana na mazungumzo ya Iran na Saudi Arabia, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, siku zote Tehran imekuwa ikitangaza utayari wake kwa ajili ya mazungumzo katika fremu ya duru za hapo kabla za mjini Baghdad, Iraq.