Khatibzadeh: Iran inasubiri majibu ya Wamagharibi katika mazungumzo ya Vienna
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, hakuna mkwamo wowote katika mazungumzo ya Vienna na kilichopo ni kwamba hivi sasa Iran inasubiri majibu kutoka kwa nchi za Magharibi zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo.
Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, mazungumzo kuhusu masuala yaliyobakia yanaendelea na kadiri Marekani na nchi tatu za Ulaya zitakavyoonesha nia njema ndivyo mazungumzo hayo yatakavyozidi kukaribia kwenye mapatano.
Akijibu swali katika mazungumzo yake hayo ya kila wiki na waandishi wa habari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia umekaribia kumalizika na kama Marekani na nchi tatu za Ulaya zitazingatia pendekezo la Iran, kuna uwezekano kukafikiwa makubaliano mapya mapema zaidi ya inavyotarajiwa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesisitiza kuwa, wakati wa kufikiwa makubaliano mapya unategemea nia na msimamo wa Marekani na pande za Magharibi na inachotegemewa kutoka kwa nchi hizo ni kufanya maamuzi ya haraka ya kisiasa ili kuharakisha kufikiwa mapatano mapya.
Akijibu swali kuhusu maamuzi gani hasa yanasubiriwa na Iran, Khatibzadeh amesema, Marekani ni nchi ambayo haina mwamana hata kidogo, hivyo kuna wajibu wa kutolewa dhamani ya kivitendo ya kuhakikisha kuwa Marekani itaheshimu sheria za kimataifa na mikataba inayoweka.
Amma kuhusiana na mgogoro wa Ukraine, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran haifurahishwi na mgogoro unaoendelea baina ya Ukraine na Russia kwani ina uhusiano mzuri na nchi zote hizo mbili.