Iran yakaribisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa na taasisi za utafiti
(last modified Sat, 05 Mar 2022 03:05:28 GMT )
Mar 05, 2022 03:05 UTC
  • Iran yakaribisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa na taasisi za utafiti

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran amesema kuwa, Tehran inakaribisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa na taasisi za kielimu na kiutafiti.

Kwa mujibu wa IRIB, Mohammad Eslami alisema hayo jana Ijumaa katika ujumbe wake kwa Mkutano wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia ya Iran na kuongeza kuwa, ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kuhakikisha kunakuweko matumizi mazuri, salama na ya kudumu ya sayansi na teknolojia ya nyuklia ni jambo muhimu sana.

Amesema, jambo hilo ni la dharura kwa ajili ya kutimiza mahitaji makubwa ya kimsingi, ya kijamii na ya kiuchumi na kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu. Aidha amesema, teknolojia ya nyuklia ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto anazokabiliana nazo mwanadamu hivi sasa hususan suala la kuweko maendeleo endelevu na kulindwa usalama wa mazingira.

 

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake huo, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran amesema, ushirikiano wa pande zote baina ya Iran na taasisi za kielimu na vyuo vikuu vya kimataifa unaweza kuongeza welewa wa pande mbili kimataifa kuhusu teknolojia muhimu mno ya nyuklia.

Eslami pia amesema, Jumuiya ya Nyuklia ya Iran ambayo ni taasisi huru isiyo ya kiserikali, ni mfano mzuri unaothibitisha kwamba taasisi zisizo za kiserikali za sayansi na teknolojia, zina nafasi muhimu katika ustawi wa sayansi na teknolojia nchini Iran na duniani kiujumla.

Tags