Iran: Kujitakia makuu Marekani kusiathiri masuala muhimu Vienna
(last modified Fri, 11 Mar 2022 03:14:33 GMT )
Mar 11, 2022 03:14 UTC
  • Iran: Kujitakia makuu Marekani kusiathiri masuala muhimu Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema masuala ya msingi na kuondolewa Iran vikwazo havipaswi kuathiriwa na tabia ya kujitakia makuu Marekani.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake ya simu na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ambapo walizungumzia masuala ibuka kwenye mazungumzo ya Vienna kati ya Iran na kundi la 4+1, ambayo lengo lake kuu ni kuondolewa Tehran vikwazo vya kiadhalimu.

Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, iwapo pande zote husika kwenye mazungumzo hayo zitatanguliza mbele uhalisia wa mambo, basi uwezekano wa kufikiwa mapatano mazuri na imara ungalipo.

Amesema maombi mapya ya Marekani kwenye mazungumzo ya Vienna hayana mantiki wala uhalali wowote, na yanakinzana na madai ya Washington ya kutaka kufikiwa haraka mapatano.

Mkutano wa Vienna

Kabla ya hapo, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran alisisitiza kuwa, Tehran inakaribisha juhudi zote za kuharakisha kufikiwa makubaliano mazuri na imara na wakati huo huo, imesimama kidete kulinda na kuchunga mistari yake myekundu hasa suala la kupewa dhamana za kutekelezwa vipengee vya makubaliano hayo na kulindwa kikamilifu manufaa ya kitaifa ya Iran.

Viongozi wa Iran na wa kundi la 4+1 wamesema kuwa, mazungumzo ya kuhuisha mapatano ya JCPOA yamefika katika hatua ya mwisho, na kwamba pande mbili zinapasa kuchukua maamuzi ya kisiasa kuhusiana na masuala kadhaa yaliyosalia. 

Tags