Kumbukumbu ya kupasishwa sheria ya kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran
Tarehe 29 mwezi Esfand mwaka 1329 kwa kalenda ya Iran inaadhimishwa kama siku ya kukumbuka kupasishwa sheria ya kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran .
Kupasishwa sheria hiyo ya kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran tarehe 29 Esfand mwaka 1329 Hijria Shamsiya inahesabiwa kuwa nukta muhimu katika historia ya kisiasa na kiuchumi na mapambano ya wananchi wa Iran kwa ajili ya kuvinusuru rasilimali na utjiri wa taifa kutoka kwenye makucha ya nchi za kibeberu.
Wakati ule ambapo Iran ilikuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi katika Asia Magharibi na mzalishaji mkuwa wa nne wa mafuta ghafi duniani baada ya Marekani, Venezuela na Urusi ya zamani, Uingereza ilipokonywa nafasi ya kunufaika na mafuta ya kusini ya Iran; na Urusi na Marekani nazo zilikuwa zikikodolea macho utajiri wa mafuta ya Iran, na ni wazi kuwa wakoloni walikuwa wakichuana kugombania rasilimali hiyo. Njama mbalimbali dhidi ya Iran ziliongezeka pale serikali ya wakati huo ya Waziri Mkuu Muhammad Musaddeq ilipotoa kipaumbele katika utekelezaji wa sheria ya kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran mnamo mwezi Aprili mwaka 1951. Mapinduzi ya Marekani na Uingereza mwezi Agosti mwaka 1953 dhidi ya serikali ya Musaddiq yalikuwa sehemu ya njama hizo.
Baada ya mapinduzi hayo, makampuni ya mafuta kama BP, Shell na makampuni ya mafuta ya California na Texas yaliingia katika medani na kuanza kuiba mafuta ya Iran ili mababeru wendelee kudhibiti mafuta ya nchi hii licha ya kutaifishwa. Hata hivyo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1357 Hijria Shamsiya (1979) mikataba yote ya nchi za ajinabi ukiwemo mkataba wa mwaka 1352 wa (Renewal of the Consortium) Ilifutwa, na kuanzia tarehe 14 mwezi Esfand mwaka 1357 Hijria shamsiya (5 Machi 1979) haki ya shughuli za kutafuta, kuchimba na kusafisha mafuta iliondolewa mikononi mwa nchi kigeni na kukabidhiwa kwa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hususan katika kipindi cha muongo mmoja uliopita sambamba na sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu la udharura wa kutekelezwa fikra ya uchumi wa kimapambano; sera ya kujiweka mbali na uuzaji nje mafuta ghafi ilipewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni asilimia 22 tu ya uzalishaji wa mafuta ghafi ambayo yangeweza kusafishwa nchini, lakini hivi sasa kiwango hicho kimefikia karibu asilimia 45, jambo ambalo linaashiria kupungua kwa mauzo ya mafuta ghafi baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Uzalishaji wa vifaa vinavyohitajika katika sekta ya mafuta, gesi na petrokemikali daima umekuwa miongoni mwa matatizo ya sekta ya mafuta ya Iran na sekta hii baada ya miaka 43 ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini imeweza kujitosheleza kwa asilimia 85 katika utengenezaji wa vifaa hivyo.
Lengo la maadui katika kuiwekea vikwazo sekta ya mafuta ya Iran lilikuwa kusimamisha uuzaji nje wa mafuta ili kuathiri uchumi wa Iran, na vilevile kudhoofisha sekta hiyo na kupunguza uwezo wa uzalishaji wa nchi kwa kuzuia uagizaji wa zana na bidhaa zinazohitajika kutoka nje ya nchi.
Kwa hivyo, uzalishaji wa mafuta wa Iran, ambao unategemea sana zana na vifaa maalumu, uliwekwa hatarini. Mara hii pia, kwa msaada wa bidii, uwezo na fikra za wataalamu wa ndani, suala la utengenezaji wa vifaa hivyo na bidhaa zinazohitajika katika sekta ya kuzalisha mafuta liliwekwa katika kilele cha malengo ya makampuni ya Iran ya baada ya Mapindui ya Kiislamu, na hadi sasa asilimia 85 ya bidhaa na vifaa hivyo vinatengezwa ndani ya nchi huku asilimia iliyobaki ikiwa inashughulikiwa.
Ugunduzi wa maeneo 65 ya mafuta na gesi, ongezeko la akiba inayoweza kuchimba ya mafuta na gesi kufikia mapipa bilioni 160, ongezeko la uzalishaji wa mafuta, ongezeko la gesi ya kuchimbwa hadi mita za ujazo trilioni 33, ugunduzi wa medani ya gesi wa Pars Kusini na kujitegemea katika uzalishaji wa petroli ni miongoni mwa mafanikio ya sekta ya mafuta ya Iran katika nyanja za utafutaji na uzalishaji, ambayo yamepatikana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.