Iran: Marekani iachane na siasa zake za kibeberu na kupenda makuu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Marekani inapaswa kuachana na siasa zake za kupenda makuu katika mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea mjini Vienna Austria na iyaangalie mazungumzo hayo katika uhalisia wake.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Hossein Amir-Abdollahian akisema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi wakati alipozungumza kwa simu na Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nia ya kweli na hamu ya kufikiwa makubaliano mazuri na ya kudumu katika mazungumzo hayo ya kuondolewa haraka vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Tehran. Hivyo Marekani inapaswa kuachana na siasa zake za kupenda makuu na kutojiamini kwani kufanya hivyo hakusaidii juhudi za kumaliza vizuri mazungumzo ya Vienna.
Itakumbukwa kuwa, awamu ya nane ya mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa kuhusu mradi wake wa amani wa nyuklia, ilianza tarehe 27 Disemba 2021. Tarehe 11 Machi 2022, Mkuu wa Sera za Kiageni za Umoja wa Ulaya aliomba mazungumzo hayo yaingie kwenye mapumziko kidogo ili timu za mazungumzo zirejee kwenye nchi zao kwa ajili ya kushauriana zaidi.
Marekani inafanya njama za kuitupia lawama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutofikiwa mwafaka katika mazungumzo ya Vienna. Lakini muda wote Iran imekuwa ikitangaza wazi misimamo yake na imekuwa ikifanya ubunifu wa kila namna kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanikiwa na haki zake zinalindwa kikamilifu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Muda wote Iran imekuwa ikitangaza msimamo wake kuwa kwanza ni kuondolewa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa kuhusu mradi wake wa nyuklia kinyume kabisa na makubaliano ya JCPOA.
Pia Iran inataka kupewa haki ya kuchunguza na kuhakikisha ni kweli vikwazo hivyo vimeondolewa. Aidha Iran inataka dhamana kwamba Marekani haitotia tena ulimi puani na haitairejeshea tena Tehran vikwazo vilivyoondolewa baada ya kufikiwa mapambano ya JCPOA.