Iran yazionya Marekani na nchi tatu za Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84280-iran_yazionya_marekani_na_nchi_tatu_za_ulaya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amezihutubu nchi tatu za Ulaya, yaani Ujerumani, Uingereza na Ufaransa pamoja na Marekani na kusema: "Mnaweza kufuata mkondo wa udiplomasia au muende kinyume chake. Sisi tuko tayari kwa machaguo hayo mawili."
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jun 01, 2022 22:53 UTC
  • Iran yazionya Marekani na nchi tatu za Ulaya

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amezihutubu nchi tatu za Ulaya, yaani Ujerumani, Uingereza na Ufaransa pamoja na Marekani na kusema: "Mnaweza kufuata mkondo wa udiplomasia au muende kinyume chake. Sisi tuko tayari kwa machaguo hayo mawili."

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo kupitia ujumbe wa Twitter na kusema: "Utawala wa Israel, kama adui nambari moja wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, inapinga mapatano ya NPT ya kuzuia silaha za nyuklia na ni utawala pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Sisi hilo tunalijua na dunia pia inalijua."

Khatibzadeh ameongeza kuwa, wakati umewadia kwa nchi tatu za Ulaya na Marekani kuacha kujifanya kuwa ziko katika usingizi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa nchi hizo tatu zinaweza kuchagua udiplomasia au kinyume chake lakini zifahamu kuwa Iran iko tayari kwa machaguo yote hayo.

Mapema Jumatano shirika la habari la Reuters lilichapisha ripoti iliyosema kuwa Marekani na nchi tatu za Ulaya,yaani Ujerumani, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zimependekeza azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

Khatibzadeh huko nyuma alikuwa ametahadharisha kuwa hatua yoyote isiyo sahihi ya Bodi ya Magavana ya IAEA itakabiliwa na jibu kali kutoka Iran na kusema bodi hiyo itabeba dhima ya yatakayotokea kutokana na kutumiwa kwake kama chombo cha mashinikizo na michezo ya kisiasa dhidi ya Iran.

Kuhusu ripoti iliyotolewa Jumatatu na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema, ripoti hiyo haikuzingatia insafu na kuna mambo ndani ya ripoti hiyo yameelezwa kwa pupa.

Sambamba na kutanabahisha kuhusu hofu iliyopo ya mashinikizo ya Wazayuni na baadhi ya pande kuutoa mkondo wa ripoti za IAEA kwenye anga ya kiufundi na kuuelekeza kwenye matashi ya kisiasa, Khatibzadeh amesema, anatumai kuwa mwenendo huo usio sahihi utarekebishwa.