Iran na Venezuela zasaini makubaliano ya ushirikiano ya miaka 20
(last modified Sat, 11 Jun 2022 11:16:09 GMT )
Jun 11, 2022 11:16 UTC
  • Iran na Venezuela zasaini makubaliano ya ushirikiano ya miaka 20

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenzake wa Venezuela, Nicolas Maduro wamesaini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano ya miaka 20, yenye lengo la kupiga jeki uhusiano wa nchi mbili hizi katika nyuga mbalimbali.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo ya ushirikiano imefanyika mbele ya marais hao wawili hapa mjini Tehran leo Jumamosi. Kwenye makubaliano hayo, Tehran na Caracas zimekubaliana kushirikiana katika nyuga za sayansi, teknolojia, kilimo, mafuta na gesi, petrokemikali, utalii na vilevile utamaduni.

Rais Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kusainiwa makubaliano hayo ya ushirikiano ya miaka 20 kunaonesha bayana kuwa, Iran na Venezuela zimeazimia kuboresha uhusiano wao wa pande mbili licha ya mashinikizo ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.

Sayyid Raisi amesema, "Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikifuatilia kuimarisha uhusiano wake na nchi huru duniani katika uga wa sera za kigeni; na Venezuela imesimama kidete mkabala wa vikwazo vya maadui na mabeberu, na imeonesha mapambano ya hali ya juu."

Raisi amesema taifa la Iran vilevile limekuwa chini ya vikwazo kwa zaidi ya miongo minne sasa, lakini wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu wamevigeuza vikwazo hivyo kuwa fursa ya kuistawisha zaidi nchi yao.

Ameeleza kuwa: Msemaji wa Ikulu ya White House (ya Marekani) amewahi kukiri kuwa mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran yamegonga mwamba, na huo ni ushindi kwa Jamhuri ya Kiislamu na pigo kwa maadui.

Rais wa Iran amesema anatumai safari ya Rais wa Venezuela hapa nchini itafungua ukurasa mpya wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili, na kwamba safari za ndege za moja kwa moja baina ya Tehran na Caracas zitakazoanza karibuni hivi, zitaandaa mazingira ya kunyanyuliwa uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya mataifa haya mawili.

Marais wa Iran na Venezuela katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari mjini Tehran

Kwa upande wake, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa, nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndizo nchi zilizoko mstari wa mbele katika kupambana na ubeberu na uistikbari duniani kutokana na kuwa lengo lao ni moja.

Rais Maduro ambaye aliwasili hapa Tehran jana Ijumaa kwa ziara rasmi ya siku mbili akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake amesema, nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinashirikiana kwa karibu katika takriban nyuga zote hususan ulinzi, uchumi na nishati.

Amedokeza kuwa, safari za moja kwa moja za ndege baina ya Tehran na Caracas zinatazamiwa kuzinduliwa Julai 18.

 

Tags