Gharib Abadi: Iran ni mhanga mkubwa wa ugaidi duniani
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Idara ya Mahakama ya Iran amesema, zaidi ya watu elfu 25 nchini Iran wamepoteza maisha kutokana na vitendo vya kigaidi; ambapo uungaji mkono wa Marekani kwa jinai zote hizo unashuhudiwa.
Kipindi cha kuanzia tarehe 27 Juni hadi Julai 3 kimepewa hapa nchini jina la " Wiki ya Kupitia na Kufichua Haki za Binadamu za Marekani". Wiki ya Haki za Binadamu za Marekani inakumbusha jinai za moja kwa moja au zile zilizofanywa kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani dhidi ya wananchi wa Iran.
Kazim Gharib Abadi Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu na ambaye pia ni Afisa wa Masuala ya Kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mhanga mkuu wa ugaidi na kwamba Marekani inatumia haki za binadamu kikamilifu kama wenzo wa kufanikisha sera zake za nje ili kutimiza malengo yake; na wakati huo huo kuzituhumu nchi nyingine kuhusu haki za binadamu ili kuzilazimisha ziige vigezo vyake kuhusu haki za binadamu.
Gharib Abadi amebainisha hayo jana katika Mkutano wa Kufichua Haki za Binadamu za Marekani uliofanyika hapa Tehran. Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama ya Iran amesisitiza kuwa, Marekani inaongoza kwa vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya nchi huru duniani na huku ikiwa imeziweka katika orodha yake ya vikwazo vya upande mmoja zaidi ya nchi 30.