Rais Rouhani aipa nishani timu ya nyuklia ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amempa nishani ya heshima Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na amewapa nishani za ushujaa Waziri wa Ulinzi na Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran kutokana na kazi kubwa ya kujivunia waliyoifanya katika kadhia ya nyuklia.
Rais Rouhani amesema kwenye sherehe hizo zilizofanyika leo kuwa, ushindi lilioupata taifa la Iran katika uga wa nyuklia na kupelekea kuanza kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na kundi la 5+1 linaloundwa na nchi sita zenye nguvu duniani, ni ushindi wa serikali zote za Iran na wananchi wote, na hauhusiani na watu fulani tu.
Vile vile amezienzi familia za mashahidi wa nyuklia na amezipa loho za shukrani familia za shahid Masoud Ali Mohammadi na Reza Qashqavi waliowakilisha familia zote za mashahidi wa nyuklia nchini.
Baada ya kupokea nishani hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, miongozo na uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na usimamiaji mzuri wa Rais ndio uliotoa mchango mkubwa wa kupatikana mafanikio hayo katika mazungumzo ya nyuklia.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 14 Julai 2015, Iran na kundi la 5+1 zilifikia makubaliano muhimu sana yaliyopelekea kufungwa faili la nyuklia la Iran na baada ya pande mbili kutekeleza ahadi zao, mpango wa nyuklia unaojulikana kwa jina maarufu la JCPOA ulianza kutekelezwa tarehe 17 Januari mwaka huu kulikokuwa na maana ya kufutwa vikwazo vya kidhulma ilivyokuwa imewekewa Iran na madola ya Magharibi.