Ayatullah Khatami: Maadui wanataka kudhoofisha umoja wa Waislamu
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa Tehran amesema maadui wanafanya juu chini kupunguza na kudhoofisha umoja wa umma wa Kiislamu kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Ayatullah Ahmad Khatami amesema hayo katika hotuba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa Tehran na kuongeza kuwa, baadhi ya mbinu zinazotumiwa na maadui kuyumbisha umoja wa Waislamu ni kujaribu kuwapotosha waachane na masuala ya kimaanawi na kumkumbuka Allah.
Ameashiria ujumbe muhimu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu na kubainisha kuwa, "Nguzo mbili muhimu za ibada ya Hijja ni Dhikr (kumtaja/kumdhukuru Allah) na umaanawi.
Imamu huyo wa muda wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran ameeleza kuwa, maadui wanafanya kila wawezalo ili kuzidogosha nukta mbili hizi katika mataifa ya Waislamu, ili wafanikishe njama zao za kuugawa umma wa Kiislamu.

Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, ujumbe wenye thamani wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mahujaji unapaswa kuzingatiwa na kutathminiwa kwa wakati muafaka.
Moja ya nukta zilizoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake kwa Mahujaji ni kuwa, nchi za Magharibi zenye kiburi zimezidi kudhoofika siku baada ya siku katika eneo hili nyeti la Asia Magharibi, na hivi karibuni katika dunia nzima.