Vikao muhimu kufanyika katika safari ya Putin na Erdogan nchini Iran
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Ankara amedokeza kuwa kutafanyika vikao viwili muhimu mjini Tehran wiki ijayo ambavyo vitahudhuriwa na marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki.
Mohammad Farazmand balozi wa Iran mjini Ankara Uturuki ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Wiki ijayo kutafanyika vikao viwili muhimu mjini Tehran. Kwanza ni kikao cha Kamati Kuu ya Uhusiano wa Iran na Uturuki na pili ni 'Kikao cha Viongozi wa Ubunifu wa Astana."
Putin na Erdogan wanatazamiwa kuwasili nchini Iran wiki ijayo kushiriki katika vikao hivyo na kufanya mazungumzo ya viongozi wa ngazi za juu wa Iran.
Balozi Farazvand amesema katika kipindi hiki nyeti na chenye kuainisha hatima ya eneo na dunia, mji mkuu wa Iran, Tehran utakuwa mwenyeji wa vikao hivyo viwili muhimu vya kimataifa ambavyo havijafanyika kwa muda mrefu.

Hivi karibuni Ikulu ya Russia (Kremlin) ilithibitisha kuwa Rais wa nchi hiyo Vladmir Putin atafanya ziara mjini Tehran ambapo atakuwa na mazungumzo na Rais wa Iran.
Dmitry Peskov Msemaji wa Ikulu ya Kremlin ameeleza kuwa, Rais Vladmir Putin Jumanne ijayo Julai 19 atafanya safari Tehran kwa lengo la kushiriki katika mkutano wa pande tatu wa Marais wa Iran, Russia na Uturuki katika fremu ya mazungumzo ya Astana kuhusiana na mchakato wa amani ya Syria.