Iran: Uhusiano wetu na Tanzania unazidi kustawi na kuimarika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, uhusiano wa Tehran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unazidi kuwa imara.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo baada ya kuonana na kuzungumza na viongozi wa ngazi za juu wa Tanzania, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametembelea Tanzania ikiwemo Zanzibar baada ya kumaliza ziara yake katika nchi ya magharibi mwa Afrika ya Mali na hiyo ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani Afrika tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Wakati wa mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Amir-Abdollahian ameashiria uwezo mkubwa wa Iran kiuchumi hasa katika nyuga za biashara, nishati, viwanda, teknolojia na vyuo vikuu na ametoa mwito wa kuondolewa vikwazo kwa mashirika na wafanyabiashara wa Iran nchini Tanzania hasa katika masuala ya visa.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ametoa mwito wa kuimarishwa mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi baina ya Iran na Tanzania na amekubali mwaliko rasmi wa kuitembelea Iran kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi. Amesema, ana matumaini ya kufanya safari hiyo ya kuitembelea Iran kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2022.
Mapema jana Ijumaa pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na Rais Hussein Ali Hassan Mwinyi wa Zanzibar na wawili hao wakasitizia udharura wa kuimarishwa ushirikiano baina ya pande mbili hasa kutokana na uhusiano wa jadi uliopo baina ya mataifa haya mawili.