Iran yaipongeza Iraq kwa kutumia hekima kuhitimisha ghasia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewapongeza wananchi wa Iraq kwa kutumia hekima kukabiliana na jaribio la uasi lililosababisha ghasia na fujo nchini humo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema, Jamhuri ya Kiislamu inataka kuliona taifa hilo jirani yake likiwa na uthabiti, huku ikipongeza kurejea kwa hali ya utulivu na amani katika nchi hiyo.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu imesisitiza kuwa, "Iran daima inataka Iraq yenye uthabiti, usalama na nguvu, na inayochangia kwa njia chanya ustawi wa kieneo."
Imesema njia pekee ya Iraq kuondokana na mgogoro wa sasa ni kupitia mazungumzo, kulinda haki za raia, na kuheshimu mchakato wa kisiasa.
Tehran imesisitiza kuwa, daima inaheshimu mchakato wa kisiasa na kisheria wa Iraq, na taasisi za nchi hiyo.
Kabla ya hapo, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza haja ya kuhifadhiwa umoja wa kitaifa wa Iraq, akisema matatizo ya nchi hiyo yanapaswa kutatuliwa kwa njia za kisheria.
Iraq imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana. Vyama hasimu vimeshindwa kuafikiana kuhusu kuundwa kwa serikali mpya, hivyo kusababisha maandamano na hujuma ya wafuasi wa makundi ya kisiasa dhidi ya bunge.
Kiongozi mashuhuri wa kidini, Muqtada al-Sadr na wafuasi wake wamezusha hali ya wasiwasi katika muda wa wiki mbili zilizopita huku maelfu ya wafuasi wake wakivamia na kulikalia bunge la nchi hiyo na kuzuia kuundwa kwa serikali karibu miezi 10 baada ya uchaguzi uliopita.