Iran yasisitiza kuondolewa vizingiti vya kifedha na kibenki
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuhusu utekelezwaji kamili wa makubaliano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Hayo yamedokezwa na Hamid Baeidinejad Mkurugenzi Mkuu wa Kisiasa na Masuala ya Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambaye ameongeza kuwa, Tehran itaendelea kufuatilia uondolewaji wa vizingiti vyote vya kifedha na kibenki ili mapatano ya nyuklia yaweze kutekelezwa kikamilifu.
Baeidinejad amebainisha kuwa, lengo kuu la mapambano na kusimama kidete taifa na serikali ya Iran katika kipindi cha miaka 12 iliyopita katika kadhia ya nyuklia ni kuhakikisha kuwa nchi hii inapata haki yake ya kimsingi ya kurutibisha madini ya urani kwa ajili ya kuzalisha nishati ya nyuklia.
Aidha amesema, ni kwa sababu ya kutetea haki hiyo yake ya kimsingi ndio Iran ikapinga maazimio yote ya Baraza la Usalama ya kutaka nchi hii isitishe kwa muda au isimamishe kabisa mpango wake wa kurutibisha madini ya urani. Amesema Iran itaendelea na msimamo huohuo wa mapambano hadi ipate haki zake zote.
Iran mara kadhaa imesisitiza kuwa vikwazo vya kiuchumi, kifedha na kibenki, viwe ni vile vilivyowekwa na Baraza la Usalama au vile vilivyowekwa na Kongresi ya Marekani au vile vilivyowekwa na serikali ya Marekani, lazima vyote viondolewe baada ya kutiwa saini makubaliano hayo. Hata hivyo Marekani imekuwa ikiweka vizingiti katika uondolewaji wa vikwazo hivyo kinyume ncha mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.