Rais Rohani: Iran haikupoteza chochote kwenye JCPOA
Rais Hassan Rohani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo kuwa, makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya nchi hii na madola makubwa duniani yalikuwa kwa manufaa ya pande zote na kwamba wanaosema Iran ilipoteza kwenye mazungumzo hayo wanapotosha ukweli wa mambo.
Rais wa Iran amesema hata nchi zilizokuwa zikipinga makubaliano hayo ya nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati sasa zimeanza kubadili misimamo na kusema yalikuwa ya manufaa kwa pande zote husika. Amesisitiza kuwa wanadiplomasia wa Iran walisimama kidete kutetea haki za taifa lao na kwamba walikuwa tayari kuondoka kwenye meza ya mazungumzo kama kungekuwa na mtazamo wowote wa kuhujumu haki za nchi yao katika uwanja wa teknolojia ya nyuklia.
Dkt. Hassan Rohani amesema hayo muda mfupi uliopita wakati akihutubia maafisa wa serikali wanaohusika na mipango na maendeleo ya taifa. Rais wa Iran amewataka maafisa hao kutumia fursa iliyojitokeza kwa ajili ya kuharakisha miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Julai 14 mwaka uliopita, Iran ilifikia makubaliano ya kihistoria na nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uchina, Russia pamoja na Ujerumani ambazo zinaunda kundi la 5+1 kuhusiana na miradi yake ya nyuklia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Iran imetakiwa kupunguza baadhi ya mambo kwenye miradi yake ya nyuklia mkabala wa kuondolewa vikwazo vya kimataifa. Tayari utekelezwaji wa makubaliano hayo umeanza na vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran vimeondolewa.