Raisi: Uingiliaji wa maajinabi hauwezi kutatua matatizo ya Asia Magharibi
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi za Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, uingiliaji huo kamwe hauwezi kuwa suluhu ya matatizo na changamoto za eneo hili.
Rais wa Iran alisema hayo jana hapa Tehran baada ya kurejea nchini kutoka Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, alikoenda kushiriki mkutano wa sita wa wakuu wa nchi wanachama wa "Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia" (SICA).
Ameeleza kuwa, "Uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya Asia unachochea zaidi hali ya mambo katika eneo, na hili lilikuwa suala kuu katika mkutano wa SICA."
Rais wa Iran amesema Marekani na nchi za Magharibi zinataka kutekeleza siasa zao za kibeberu katika eneo, na kwamba kuwepo ushirikiano wa pamoja na amani barani Asia hakuendani na maslahi ya nchi za kibeberu.
Kadhalika Rais wa Iran akiwa Astana alikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Kazakhstan, na kutilia mkazo suala la kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili wa nchi mbili hizi jirani katika nyuga tofauti.
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuambia mkutano wa sita wa wakuu wa nchi wanachama wa "Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia" (SICA) kuwa, dunia ya leo inahitaji kuliko wakati wowote ule mchango athirifu na madhubuti wa taratibu zinazobuniwa kikanda.
Nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda ni Iran, Kazakhstan, Afghanistan, Pakistan, Korea Kusini, China, Russia, India, Palestina, Mongolia, Kyrgyzstan, Uzbekistan, Tajikistan, Jamhuri ya Azerbaijan na Thailand.