Kombe la Dunia, Iran yaipongeza Qatar, yasisitiza kuimarishwa uhusiano wa pande zote
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza Qatar kwa kuendesha vizuri mashindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu 2022 na kusisitizia wajibu wa kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Doha katika nyuga zote.
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kunukuu mazungumzo ya simu aliyofanya Rais Ebrahim Raisi na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Aal Thani ambapo sambamba na kumpongeza kwa kuandaa, kusimamia na kuendesha kwa njia bora mashindano hayo, Rais wa Iran amehimiza kufuatiliwa kwa karibu na kwa kina makubaliano yanayofikiwa baina ya nchi mbili na kuhakikisha yanafanikishwa kwa ufanisi mkubwa.
Rais Raisi amempongeza pia Amir wa Qatar kwa kuhakikisha anachunga matukufu na mafundisho ya Uislamu katika mashindano hayo yanayoendelea hivi sasa huko Qatar.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia uhusiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Doha katika nyuga mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kusema kuwa, uhusiano huo utaimarika zaidi iwapo makubaliano na maafikiano yote yatafuatiliwa na kutekelezwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Aal Thani amesema katika mazungumzo hayo ya simu kwamba uhusiano wa Qatar na Jamhuri ya Kiislamu ni wa muda mrefu, ni wa kirafiki na ni wa kidugu. Ameongeza kuwa, Doha ina hamu ya kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wake wa kiistratijia na Tehran.
Amir wa Qatar amehimiza pia wajibu wa kufuatiliwa na kutekelezwa kivitendo makubaliano yote yanayofikiwa baina ya pande mbili.