Jan 02, 2023 11:29 UTC
  • Baraza la Maulamaa la Nigeria: Mauaji ya Jenerali Soleimani ni jinai

Baraza la Maulamaa wa Kiislamu Nigeria, limelaani vikali mauaji ya kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Luteni Jenerali Qassem Solaimani na kusema mauaji hayo yaliyotekelezwa na Marekani ni jinai.

Katika mahojiano na Shirika la Habari la Iran Press jana Jumatatu mjini Abuja, Mwenyekiti wa Baraza la Maulamaa wa Nigeria Sheikh Dan'azumi Musa Tafawa Balewa amebaini kuwa mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Solaimani yaliyotekelezwa na Marekani ni "unafiki wa wazi wa sera ya Marekani ambao unadhoofisha haki za kweli za binadamu."

Mhubiri huyo mkuu wa Kiislamu wa Kisunni nchini Nigeria amesema: "Ninafahamu kilichotokea (mwaka wa 2020), ambapo Marekani ilianzisha shambulio la kihalifu, shambulio la kigaidi dhidi ya mtu muhimu kama Luteni Jenerali Qassem Soleimani, na wengine wengi ulimwenguni kote ambao walikuwa wakitetea haki za binadamu."

Aidha amesema mauaji ya Shahidi Soleimani yalikuwa maafa si kwa watu wa Iran na Iraq tu, bali kwa Waislamu wote duniani na watu wote wanaodhulumiwa duniani."

Aidha amezikosoa Marekani na waitifaki wake hasa Israel madola ya Magharibi kwa kuwatia moyo magaidi kama Boko Haram nchini Nigeria na makundi mengine ya kitakfiri kama ISIS au Daesh katika nchi za Kiislamu.

Lt. Jenerali Soleimani, ambaye alikuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Naibu Kamanda Jeshi la Kujitolea la Wannachi wa Iraq (PMU) Abu Mahdi al-Muhandis, na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mapema  Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.

Ikulu ya White House na Pentagon zilitangaza kuwa Marekani ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi  na kuthibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.

Mipango mbalimbali imepangwa kutekelezwa nchini Iran, Iraq na nchi nyingine kadhaa ili kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha Jenerali Soleimani, al-Muhandi na wanajihadi wenzao.

 

Tags