Jan 02, 2024 16:45 UTC
  • Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani
    Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani

Hamjambo na karibuni kujiunga nami katika makala hii maalumu ya kukumbuka kuuawa shahidi Kamanda wa Kiislamu, Haj Qassem Soleimani, fahari na kinara wa Iran katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS). Kamanda huyu shujaa aliuawa shahidi katika shambulio la kikatili na kigaidi la ndege za kivita za Marekani huko Iraq.

Mmoja wa waliokuwa katika moja ya vikao vya mwisho vya Kamanda Qassem Soleimani anasimulia yaliyojiri.

Ilikuwa Alhamisi, Januari 2, 2020 mjini Damascus, Syria na watu wote walikuwa wanamsubiri kamanda. Alifika  saa mbili asubuhi. Baada ya salamu, alianza mkutano.

Kila mtu alipaswa kuandika. Kuandika kila alichokuwa akisema.

Tumezoea kuandika maelezo, lakini Haj Qassem alisisitiza tuandike yote aliyokuwa akiyasema. Hatua kwa hatua tuliendelea.

Mpango wa kazi ya miaka mitano ijayo

- Mpango wa kila kundi la muqawama katika miaka mitano ijayo

- Jinsi ya kushirikiana na kila mmoja

Karatasi imejaa nukta muhimu za Kamanda. Hatukuwa tumewahi kuona kiwango kikubwa kama hiki cha maudhui katika mkutano. Kamanda Soleimani alikuwa makini sana wakati wa kufanya mikutano. Hakuna aliyethubutu kumkatiza; Lakini wakati huu hali ilikuwa tofauti. Tulipouliza maswali, alisema kwa utulivu: "Usiwe na haraka." Acha nimalizie."

Wakati wa adhana ulifika na tulikatiza mkutano na tukaenda kuswali. Baada ya hapo tuliendelea na mkutano. Haj Qassim alisema kila kilichokuwa moyoni mwake nasi tulikiandika. Saa tisa alasiri alitangaza mwisho wa mkutano kwa kumswalia Mtume SAW.

Tulimsindikiza hadi kwenye gari tulilokuwa tukilisubiri. Alikuwa anaelekea Beirut. Alitaka kukutana na Seyyed Hassan Nasrallah, kiongozi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Abu Mahdi Al-Muhandis

Wakati alipokutana na Seyed Hassan Nasrallah, Seyed alimwambia: "Vyombo vya habari vya Marekani vinakulenga wewe. Wanaonekana kuandaa mazingira ya kuuawa kwako. Haj Qassim alitabasamu tu. Alirejea Syria usiku. Usiku wa Alhamisi, aliondoka kuelekea uwanja wa ndege wa Damascus ili kutoka hapo aelekee Baghdad, Iraq. Marafiki zake walisisitiza kwamba asiende safari hiyo kutokana na hali ya wasiwasi nchini Iraq, lakini alimwambia Seyyed Hassan Nasrallah: "Lazima niende Baghdad mimi mwenyewe." Haj Qasim alipaswa kufikisha ujumbe kwa waziri mkuu wa wakati huo wa Iraq. Saa sita usiku, ndege iliruka kutoka Damascus kuelekea Baghdad.

Saa saba na dakika 20 usiku wa manane Ijumaa, Januari 3, 2020

Ndege ya Haj Qasim ilitua katika uwanja wa ndege wa Baghdad. Abu Mahdi Al-Muhandis alifika uwanjani kumkaribisha.

Wanajihadi hawa wawili marafiki walikumbatiana kwa bashasha ya kawaida, kisha wakaondoka uwanja wa ndege kwa magari mawili ... lakini muda mfupi baadaye, magari yote mawili yalilengwa wakati huo huo na shambulio la kombora la ndege zisizo na rubani za Marekani na Kamanda wa ngazi za juu Uislamu na wenzake wakauawa shahidi na kuelekea peponi...

Awali, vyombo vya habari vilichapisha habari zisizo rasmi kuhusu kuuawa shahidi kwa Jenerali Haj Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Kiislamu IRGC, na Abu Mahdi Al-Muhandis, naibu kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, maarufu kama Hashd al-Shaabi wa Iraq. Saa moja baadaye, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza rasmi kuwa Jenerali Soleimani aliuawa kwa amri ya Rais Trump wa Marekani. Baadaye ilisemekana kuwa vyombo vya kijasusi na usalama vya baadhi ya nchi mdogo na za kisaliti katika eneo, utawala wa Kizayuni wa Israel na kampuni binafsi ya mamluki ya  Blackwater walikuwa washirika wa Marekani katika shambulio hilo la kiwoga.

 

Utawala wa Kizayuni na Wamarekani walijaribu kumuua Jenerali Soleimani mara nyingi huko Lebanon, Syria na Iraq. Ndege zisizo na rubani za Marekani zilikuwa zikiruka kila mara juu yake, na kwa kutoa taarifa kwa magaidi ambapo makazi ya Haj Qasim yalitambuliwa na kulengwa mara kadhaa. Mara moja katika kijiji cha Bashkawi cha Aleppo huko Syria, walimshambulia kwa risasi za moja kwa moja; Wakati mwingine, kusini mwa Aleppo, gari lake lililengwa kwa makombora, mahali pengine, alilengwa kwa risasi za mlenga shabaha maalumu kaskazini mwa Hama, gaidi mshambuliaji wa kujitoa mhanga wa makundi ya wakufurishajii alijilipua karibu na Haj Qasim, na huko Abu Kamal, mlenga shabaha wa kundi la kigaidi la ISIS alimfyatulia risasi lakini ikamkosa. Vipande vya ilipofika risasi vilianguka kwenye kichwa, uso na macho ya Haj Qasim. Kila moja ya matukio haya yangeweza kusababisha kuuawa kwake shahidi. Lakini mapenzi ya Mwenyezi Mungu yalikuwa kwamba Haj Qasim auwawe shahidi sio na gaidi wa kawaida, bali kwa amri ya mtu muovu zaidi duniani, yaani, Donald Trump, rais wa Marekani wakati huo. Kwa sababu jihadi yake ilikuwa kubwa, kifo chake cha kishahidi kilikuwa kikubwa pia.

Habari hizo za kuuawa shahidi zilipoifikia Syria, mmoja wa marafiki zake alikwenda kwenye makazi ya Haj Qasim. Waraka aliokuwa ameuandika kwa mkono wake ulikuwa karibu na kioo: Na unasomeka hivi.

Mwenyezi Mungu nipokee

Ewe Mwenyezi Mungu, napenda kukuona

Maandishi hayo yalimfanya Mousawi ashindwe kusimama na kupumua.

Hapo palipatikana pia maandishi mengine yaliyokuwa yametiwa saini na yaliyoandikwa: Alhamdulillah, Mola wa walimwengu. Na mara mbili zaidi, aliandika maneno haya "Ewe Mwenyezi Mungu, nipokee nikiwa mtakasifu. Ni kana kwamba alitaka kuhakikisha utambulisho wake unabainika wazi na pasiwe na shaka. Wanajihadi wenzake walipoona maandishi hayo ndio kwanza walitambua kwamba safari hii ilikuwa ni safari ya mwisho ya Haj Qassim hapa duniani.

Kwa kuamuru kuuawa kwa Jenerali Qassem Soleimani, mmoja wa makamanda mashuhuri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Trump alitenda jinai ambayo marais wa kabla yake hawakuthubutu hata kuifikiria kutokana na matokeo yake. Haj Qassem Soleimani ndiye aliyekuwa mhimili mkuu wa mapambano dhidi ya magaidi wakufurishaji wa makundi kama vile ISIS au Daesh. Katika moja ya mikutano yake na Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq, Haider al-Abadi mwaka 2014, Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama alisema kuhusu Jenerali Soleimani: "Yeye ni adui wangu, lakini nina heshima ya kipekee kwake."

Katika moja ya mikutano yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Zarif, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry alisema: "Kwa mara moja, ningependa kumuona Qassem Soleimani kwa karibu." Zalmay Khalilzad, balozi wa zamani wa Marekani nchini Afghanistan pia alizungumza kumhusu na kusema: "Pamoja na kuwa Marekani inamtuhumu Soleimani kwa kuchochea vita, lakini amekuwa akifanya kazi kwa ajili ya kuleta amani na alijitahidi ili kufikia malengo yake."

Maoni haya yanaashiria kwamba kamanda huyo wa ngazi za juu wa Iran, Luteni Jenerali Soleimani, alikuwa anajulikana na serikali ya Marekani na alikuwa na mchango mkubwa sana katika kutatua matatizo ya eneo la Asia Magharibi. Kwa hiyo, kwa kuliweka jina la Qassem Soleimani katika orodha ya magaidi, Trump aliamuru kamanda huyo pamoja na Abu Mahdi Al-Muhandis kamanda wa Hashd Al Shaabi kuuawa shahidi wakati wakiondoka kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad. Ugaidi  huu ulijiri wakati Kamanda Soleimani alipokuwa anaelekea Baghdad kwa mwaliko rasmi wa Waziri Mkuu wa Iraq. Kuuawa shahidi jenerali kipenzi cha Wairani kulisababisha wimbi la hasira dhidi ya Trump na serikali yenye kiburi ya Marekani nchini Iran. Miili ya Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi Al-Muhandis na wanajihadi wenzao ilizikwa Iraq na Iran kwa fahari na adhama isiyoelezeka. Uwepo wa watu milioni kadhaa katika mazishi ya wanajihadi hao uliibua mshangao kote ulimwenguni.

Mashahidi Qassem Soleimani na Abu Mahdi Al Muhandis

Hata hivyo, ni kana kwamba kifo cha kishahidi kilikuwa mwanzo wa uwepo wa kiongozi huyu mkuu miongoni mwa mataifa na kuendelea kwa njia na harakati yake. Leo, maadui wamegundua kuwa uamuzi wa kumuua Kamanda Soleimani ulikuwa kosa la kimkakati kwa Wamarekani. Kwa mauaji hayo ya uoga, Kamanda Soleimani amekuwa hadithi ya kusisimua kwa marafiki wote wa Iran na wanaopinga madola yenye kiburi na ubeberu. Alipumua roho mpya katika makundi ya muqawama au mapambano ya Kiislamu katika ngazi ya kikanda na kuongeza hisia ya mshikamano wa kitaifa katika jamii ya Iran.

Na hii ndio sifa ya shahidi na athari ya kifo cha kishahidi; kwa hakika madola yenye kiburi hayawezi kudiriki mantiki hii. Hakuna itikadi ya kupenda mali na mambo ya kidunia inayoweza kuwaalika wafuasi wake kujitolea bila kutarajia malipo. Kwa sababu kigezo na kipimo chao pekee ni maslahi binafsi.

Lakini kujitoa mhanga na kujitoa uhai kunaweza tu kuhalalishwa katika itikadi au imani ambazo, zaidi ya maisha ya hapa duniani, zinaamini uzima wa milele wa Akhera pia. Mtu anaweza kuwa mwenye kujitolea muhanga iwapo tu anaamini katika furaha ya juu kwa ajili yake mwenyewe baada ya kifo na hivyo huweza kujitoa mwenyewe ili kufikia nafasi ya juu ya ukaribu na Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, kukubali kufa shahidi, ambacho ni kilele cha kujitolea mhanga, kunaweza tu kufurahiwa na mtu anayeamini ulimwengu wa ghaibu na Akhera. Katika utamaduni wa Uislamu, Shahidi ni mtu aliye kwenye njia ya ukweli na wema na  huwaka kama mshumaa ili wengine wasalie kwenye nuru yake na kupata faraja. Hii ndio sababu kufa shahidi ni tukio takatifu kwani ni kujitolea muhanga ukiwa una ufahamu kamili kuhusu njia hii takatifu. Mashahidi ni chanzo cha maisha ya kiroho na ustawi wa jamii. Aidha mashahidi wanafanya ukweli uonekane na kuiondoa jamii kutoka katika mkwamo, kinamasi na kutengwa. Katika barua ya mwisho ambayo shahidi Qassem Soleimani alimwandikia binti yake, anaandika kuhusu matakwa yake makubwa ya kufa shahidi akisema:

"Fatima kipenzi changu! Ninakuandikia kurasa hizi chache, kwa sababu najua unanipenda kitakatifu; Sijui kwa nini ninakuandikia maneno haya, lakini nahisi kuwa katika upweke wa maisha yangu, nahitaji kufungua moyo wangu kwa mtu ...

Ewe Mwenyezi Mungu, nilijaribu kwa wakati huu kwa miaka 30. Kwa wakati huu, nawapenda wapinzani wote. Nimeondoa majeraha, nimetuma wapatanishi. Mandhari haya ni mazuri kiasi kikubwa! Hakika ninaupenda  wakati huu...

Katika kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa nne wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, tunashuhudia kuibuka mwelekeo mpya wa ushawishi wa kumbukumbu, jina, mawazo na maadili ya hali ya juu ya shahidi huyo mwenye thamani katika eneo hili na dunia nzima. Shahidi Soleimani ndiye ukweli wa sasa unaobubujika katika jamii inayopinga madola yenye kiburi na ya kiberu. Kuchukua hatua katika njia aliyoiweka Shahidi Qassem Soleimani huleta matumaini, kujiamini, ujasiri, uvumilivu na ushindi. Mwenyezi Mungu Amrehemu

 

 

 

Tags