Kiongozi Muadhamu amuenzi Shahidi Soleimani, asema daima alifikiria kuhuisha Muqawama
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesifu na kukutaja kuwa ni kwa kipekee kujitolea kwa kamanda mkuu wa Iran wa kupambana na ugaidi, Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, ambaye aliuawa mwaka 2020 akiwa pamoja na wanajihadi wenzake katika shambulio la kigaidi la ndege isiyo na rubani ya Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.
Ayatullah Khamenei ameeleza haya mapema leo katika mkutano na kundi la familia za mashahidi Walinzi wa Haram, mashahidi wa Muqawama na wanaharakati wa mapambano kabla ya kumbukumbu ya kutimia mwaka wa tano tangu kuuliwa shahidi Jenerali Soleimani, tarehe 3 Januari.
Kiongozi Muadhamu amesema, mkakakati wa siku zote wa Shahidi Qassem Soleimani ulikuwa kuhuisha Mhimili wa Muqawama. Ayatullah Khamenei ameeleza nafasi na mchango wa kamanda mkuu huyo wa Iran katika vita dhidi ya ugaidi kuwa "usio na kifani" na akasema, kujitolea na kazi zilizofanywa na Shahidi Soleimani zinapasa kubaki katika mafundisho yetu ya kisiasa."

"Kuyalinda maeneo matukufu ilikuwa kanuni kwa Shahidi Soleimani, ambaye mara kwa mara aliitaja Iran kama "haram tukufu,"" amesema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: "Kama mashahidi wasingesabilia maisha yao, kama mapambano haya yasingekuweepo, na kama Haj Qassem Soleimani asingezungka milima na majangwa ya eneo hili kwa ushujaa…, basi leo hii kusingekuwa na dalili ya maeneo haya matakatifu."
Ayatullah Khamenei ameahidi kuwa harakati hii adilifu hatimaye itaibuka na ushindi na kusisitiza kuwa, matukio ya miaka michache iliyopita na harakati za kuyahami na kuyalinda maeneo matakatifu huko Iraq, Syria na katika eneo zima la Asia Mgaharibi yanathibitisha kwamba Mapinduzi ya Kiislamu yako imara."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Lebanon na Yemen kuwa nembo za mapambano na akasema nchi hizo lazima zitaibuka na ushindi.
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema vituo vya Marekani nchini Syria vitakanyagwakanyagwa chini ya miguu ya vijana wa Syria. Amesema kuendelea kuwepo wavamizi huko Syria ni jambo lisilokubalika na kwamba: "Syria ni ya Wasyria wenyewe; na waliovama ardhi ya nchi hiyo bila shaka siku moja watalazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano ya vijana shupavu wa nchi hiyo."