Baqeri Kani: Iran imeshikamana na misimamo yake katika mazungumzo ya kuondolewa vikwazo
Mkuu wa timu ya Iran ya kufanya mazungumzo ya nyuklia amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeshikamana vilivyo na misimamo yake katika mazungumzo ya kuondolewa vikwazo.
Ali Baqeri Kani amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, mazungumzo ni mchakato na si kitu cha kumalizika siku moja au mbili. Mazungumzo ya kuondolewa Iran vikwazo vya kidhalimu yanaendelea na hakuna mkwamo katika mchakato huo.
Baqeri Kani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, asili ya mazungumzo haijaguswa na imehifadhiwa hadi hivi sasa.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kushikamana na misimamo yake ya kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa kinyume cha sheria na itaendelea kusimama imara kupigania haki zake kwenye mazungumzo hayo.
Aidha amesema: Mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo hayo ni kuondolewa vikwazo ambavyo rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alivirejesha baada ya kuondolewa kufuatia kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 ikiwemo pia Marekani.
Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa vile vile amesisisiza kuwa, inabidi vizuizi na vikwazo vyote vya kiuchumi ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinyume cha sheria, viondolewe.