Amir-Abdollahian: Uhusiano wa Iran na Uturuki upo katika mkondo sahihi
(last modified Tue, 17 Jan 2023 13:15:08 GMT )
Jan 17, 2023 13:15 UTC
  • Amir-Abdollahian: Uhusiano wa Iran na Uturuki upo katika mkondo sahihi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema uhusiano wa pande mbili wa Jamhuri ya Kiislamu na Uturuki upo katika mkondo sahihi.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo Jumanne katika mazungumzo yake na Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje ya Uturuki mjini Ankara na kuongeza kuwa, Iran inaitazama Uturuki kama mmoja wa majirani wenye mahusiano mazuri na Jamhuri ya Kiislamu.

Abdollahian ameeleza bayana kuwa, lengo la safari yake nchini Uturuki ni kujadili pia masuala mbali mbali ya kieneo likiwemo eneo la Asia Magharibi, Caucasia Kusini, pamoja na masuala ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, serikali ya Rais Ebrahim Raisi inaichukulia kwa uzito sera ya ujirani mwema sambamba na stratajia ya kuimarisha uhusiano wa Iran na nchi za Mashariki.

Abdollahian (kushoto), Rais Erdogan na Cavusoglu

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo katika ziara yake hiyo.

Katika miezi ya karibuni, viongozi wa Iran na Uturuki wamekutana katika vikao vya pande mbili au kupitia mazungumzo ya simu ambapo pande mbili zimetilia mkazo umuhimu wa uhusiano wa nchi mbili katika nyanja za kiuchumi na ushirikiano wa kieneo kwa lengo la kimarisha usalama na kuzuia mivutano ya aina yoyote. Pamoja na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zinahitilafiana katika baadhi ya masuala.